88. Tofauti kati ya kumuomba aliye hai na mbele yako na kumuomba msaada asiyekuwa huyo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mlango wa kumi na tano

Tofauti kati ya kumuomba msaada aliye hai na mbele yako na kumuomba msaada asiyekuwa huyo

Washirikina wana hoja tata nyingine tena. Nayo ni yale aliyoyasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba watu siku ya Qiyaamah watamuomba msaada Aadam, kisha Nuuh, kisha Ibraahiym, kisha Muusa kisha ´Iysaa. Wote watatoa udhuru mpaka watapoishia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanasema:

“Hii ni dalili ya kwamba kuomba msaada mwengine asiyekuwa Allaah sio shirki.”

Tunajibu kwa kusema: “Ametakasika yule ambaye Amezipiga muhuri nyoyo za maadui Wake. Kwa hakika kuomba msaada viumbe kwa yale mambo wayawezayo, hatulipingi. Kama alivyosema (Ta´ala) katika kisa cha Muusa:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ

“Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake, Muusa akampiga ngumi akamuua.” (28:15)

Hali kadhalika ni kama jinsi mtu anaweza kumuomba msaada mwenzie katika vita au mfano wa hilo kwa kitu ambacho anakiweza kiumbe. Na sisi tumepinga kuomba msaada katika ´ibaadah kitu ambacho wanakifanya katika makaburi ya mawalii, au katika kutokuwepo kwao, pindi wanapoomba mambo ambayo hawayawezi isipokuwa Allaah pekee.

MAELEZO

Hoja tata nyingine tena ni kwamba wanaona kwamba kumuomba msaada asiyekuwa Allaah sio shirki. Amejibu hili kwa njia mbili:

1 – Aina hii ya uombaji msaada ni kumuomba kiumbe msaada katika jambo analoweza kulifanya. Aina hii haipingwi. Amesema (Ta´ala) alipokuwa anaelezea kisa cha Muusa:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ

“Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake, Muusa akampiga ngumi akamuua.”

2 – Watu hawakuwaomba Mitume hawa watukufu kuwaondoshea shida. Wamewaomba wawashufaie mbele ya Allaah (´Azza wa Jall) ili awaondoshee shida hii. Kuna tofauti kati ya kumuomba kiumbe msaada ili akuondoshee dhara na kumuomba kiumbe akushufaie mbele ya Allaah ili akuondoshee dhara hili.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 96-97
  • Imechapishwa: 28/11/2023