88. Mfano wa matendo yaliyoharamishwa katika makaburi

Baadhi ya watu wetu waliowapoteza ndugu zao wamejishughulisha na kuyajengea makaburi yao, kuyatia mawe, kuyatia chokaa, kuyajengea udongo, kuyapamba, kuyaremba na kupanda aina mbalimbali za majani juu yake. Mara nyingi wanayaendea makaburi hayo kila alhamisi. Wanazipeleka familia na ndugu zao na aina mbalimbali ya chakula huko. Wanafikiri kuwa kitu hicho kinawakurubisha mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Huenda wakasema katika mambo hayo wanaliwazika. Hawajui kuwa mambo haya ni katika Bid´ah zenye kuchukizwa zilizokatazwa na kwamba ni katika Bid´ah pia kuyaadhimisha makaburi, kuyawekea mawe na chokaa na kuyajengea makuba juu yake. Yote haya ni katika Bid´ah walizochukia Salaf na wanachuoni. Ni jambo linaenda kinyume na Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Abu Daawuud na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa Jaabir ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuyatia chokaa makaburi na kuyajengea. at-Tirmidhiy ameongeza katika upokezi wake ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza vilevile kuandika na kuyakanyaga makaburi. at-Tirmidhiy amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh. Katika upokezi wa Abu Daawuud mna ya kwamba imekatazwa kuyakalia makaburi pia.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) kwa kazi ya kutoacha sanamu lolote isipokuwa aliharibu na kuyasawazisha makaburi yote yaliyoinuliwa. Abul-Hayyaaj al-Asdiy amesimulia:

“´Aliy alinambia: “Nisikutume katika kazi aliyonituma Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Nenda na usiache sanamu lolote isipokuwa uliharibu wala kaburi lililoinuliwa isipokuwa ulisawazishe.”

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy.

Ni Sunnah kuyasawazisha makaburi haya yaliyoinuliwa, yaliyowekewa mawe, udongo na chokaa.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza vilevile kuandika juu ya makaburi, kuyafanya ni mahala pa kuswalia na kuweka mataa juu yake. Aliyakemea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mambo hayo kwa ukali kabisa mpaka akafikia kuwalaani wale wenye kufanya matendo hayo. Amekataza kuswali kwa kuyaelekea makaburi na kulifanya kaburi lake ni mahapa pa kuswalia au ni sehemu ya kutembelea mara kwa mara.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 189
  • Imechapishwa: 30/11/2016