Imependekezwa kusoma Qur-aan kwenye kaburi. Imesihi kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba aliusia atapozikwa asomewe mwishoni mwa al-Baqarah. Maoni yanayojulikana kwa Imaam Ahmad ni kwamba haikuchukizwa kusoma Qur-aan makaburini na kwenye kaburi. Maoni haya yamechaguliwa na Abu Bakr ´Abdul-´Aziyz, al-Qaadhwiy na kundi katika watu wetu [Hanaabilah]. Kitendo hichi kinafanywa na watu mpaka hii leo. Mwandishi wa al-Mustaw´ab amesema:

“Haikuchukizwa kusoma Qur-aan kwenye kaburi. Ahmad (Rahimahu Allaah) mwanzoni alikuwa akichukizwa na baada ya hapo akajirejea katika maoni hayo na kusema kwamba mwenye hekima anatakiwa kusoma baada ya kukataza kitendo hicho. Baadhi ya watu wetu [Hanaabilah] wameshikamana na maoni yake ya kwanza ya kwamba imechukizwa na kusema kuwa Ahmad ana maoni mawili katika suala hili.”

Kisha akasema:

“Akimpa yule maiti thawabu [za kisomo] zitamnufaisha.”

Haya ndio maoni vilevile ya Hanafiyyah. Lakini hata hivyo wametofautiana kama kitendo hicho kimependekezwa au kimeruhusiwa tu.

Imepokelewa ya kwamba Ahmad hakuchukizwa na kisomo wakati wa kuzika tofauti na wakati mwingine. Imepokelewa vilevile ya kwamba amechukizwa na kitendo hicho moja kwa moja. Maoni haya yamechaguliwa na ´Abdul-Wahhaab al-Warraaq na Abu Hafsw al-´Ukbariy. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Wengi wamepokea kutoka kwa Imaam Ahmad kuwa imechukizwa. Haya ndio maoni ya Salaf wengi na marafiki waliotangulia wa Ahmad kama mfano wa al-Marwaziy na wengineo.”

Ibn ´Aqiyl na Ibn-ul-Munajjaa amesema:

“Imechukizwa kusoma Qur-aan makaburini kwa kuwa pako najisi kama chooni.”

Baadhi ya wenzetu [Hanaabilah] wamesema kuwa al-Khallaal amesema:

“Madhehebu ya Ahmad yana maoni moja tu juu ya suala hili nayo inasema kuwa haikuchukizwa kusoma Qur-aan kwenye kaburi.”

Hata hivyo kusoma kwenye kaburi ni jambo halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah wake na Allaah ndiye anajua zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 184-185
  • Imechapishwa: 26/11/2016