82. Muhammad alimuona Mola wake mara mbili

80 – Amesema tena:

”Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake mara mbili.”[1]

[1] Haya yamesihi na kuthibiti kutoka kwa Ibn ´Abbaas, lakini ni masimulizi yake. Ameyapokea Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” , uk. 131. Vivyo hivyo ameyapokea Muslim kwa tamko lisemalo:

”Amemuona kwa moyo wake.”

Kadhalika ameyapokea Ibn Khuzaymah kupitia njia nyingine, kutoka kwa Ibn ´Abbaas. Muslim amempokea kupitia njia nyingine ya tatu kwa tamko kwa mnasaba wa Aayah isemayo:

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

”Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona. Je, mnambishia juu ya yale aliyoyaona? Na kwa hakika amemuona katika uteremko mwingine.” (53:11-13)

 ”Amemuona kwa moyo wake mara mbili.”

Ibn Khuzaymah pia ameipokea kwa ufupi.

Hapa haitakiwi kusema kuwa masimulizi ya Ibn ´Abbaas yana hukumu sawa na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu mlango huu haifai kwa mtu kusema kwa ijtihaad yake. Maoni yangu ni kwamba tafsiri yake ya Aayah ni dalili kubwa kabisa inayoonyesha kuwa alitamka hivo kutokana na ijtihaad yake mwenyewe, na si jambo lenye hukumu moja na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu kuna tafsiri nyingine, ambayo ni Swahiyh, inayosema kinyume chake. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

”Mimi ndiye wa kwanza katika ummah huu niliyemuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo na akasema: ”Hakika hapana vyengine alikuwa ni Jibriyl. Sikumuona katika umbo lake ambalo ni la asili isipokuwa mara hizi mbili tu. Nilimuona akishuka kutoka mbinguni. Ukubwa wa uumbwaji wake ulifunika vyote vilivyomo baina ya mbingu na ardhi.” (al-Bukhaariy (4855) na Muslim (177))

Kumepokelewa mfano wake, lakini kwa kifupi, kutoka kwa Abu Hurayrah, kwa mnasaba wa Aayah isemayo:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

”Na kwa hakika amemuona katika uteremko mwingine.”

”Alimuona Jibriyl.”

Masimulizi haya yana nguvu zaidi kuliko masimulizi ya Ibn ´Abbaas kwa sababu yanaafikiana na Hadiyth ya ´Aaishah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ibn Khuzaymah amepokea katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd”, uk. 133-134, amepokea Hadiyth nyingine inayotilia nguvu kupitia kwa Ibn Mas´uud, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa cheni ya wapokezi nzuri.

  • Mhusika: aam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 104
  • Imechapishwa: 01/07/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy