Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ile Hadiyth Swahiyh kuhusu Khawaarij inayosema:

“Hivi kweli hamniamini ilihali naaminiwa na Yule aliye mbinguni? Najiwa na khabari za mbinguni asubuhi na jioni.”[1]

MAELEZO

Khawaarij ni kipote kilichofanya uasi dhidi ya waislamu. ´Aqiydah yao ni kuwa hawaoni kufaa kuwasikiliza na kuwatii watawala. Wanawakufurisha waislamu na kuhalalisha damu zao. Ni kipote kibaya ambacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuwaua popote watakapopatikana.

Mbegu zao zilianza kuota kipindi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Siku moja wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akigawa ngawira, bwana mmoja alimwambia:

”Ee Muhammad, fanya uadilifu!” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ” Hivi kweli hamniamini ilihali naaminiwa na Yule aliye mbinguni? Najiwa na khabari za mbinguni asubuhi na jioni.”

Bi maana Allaah amemwamini juu ya Wahy. Ni vipi viumbe wasimwamini katika kugawanya ngawira ilihali Allaah (´Azza wa Jall) amemwamini juu ya kufikisha Wahy na Ujumbe? Hii ndio ´Aqiydah ya Khawaarij – hawakumsalimisha mpaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati alipoondoka bwana yule, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

”Watajitokeza watu kupitia bwana huyu ambao wataisoma Qur-aan pasi na kuvuka mitulinga yao. Watatoka katika dini kama ambavyo mshale unatoka katika upinde wake. Watawaua waislamu na kuwasalimisha washirikina. Endapo nitakutana nao basi nitawaua kama walivyouliwa kina ´Aad.”

Kwa sababu ni kipote kibaya kinachosababisha uasi, kinafarikisha waislamu, kinawakufurisha waislamu na kinazihalalisha damu zao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa wanawaua waumini na kuwasalimisha washirikina. Haijawahi kutambulika hata siku moja kuwa Khawaarij wamewaua makafiri – wao wanawaua waislamu tu.

[1] al-Bukhaariy (3610, 3344, 4351 na 7433), Muslim (1064) na Abu Daawuud (4764).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 119-120
  • Imechapishwa: 25/08/2024