81. Wakati Ibn ´Abbaas anaposema kuwa Mtume alimuona Mola wake

79 – Ibn ´Abbaas amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Nimemuona Mola wangu (´Azza wa Jall).”

Cheni yake ya wapokezi ni yenye nguvu[1].

[1] Mtunzi (Rahimahu Allaah) ameangalia udhahiri wa cheni ya wapokezi na hivyo akaitia nguvu. Ameisimulia kupitia kwa Ahmad, ambaye amesema: Aswad ametuhadithia: Hammaad bin Salamah ametuhadithia, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas. Wasimulizi wake wote ni wenye kuaminika na ni wanaume wa Muslim. Hata hivyo kuna kitu kwa Hammaad bin Salamah, pamoja na utukufu wake, kupokea kwake kutoka kwa wengine wasiokuwa Thaabit. Ndio maana Muslim hakupokea kutoka kwake isipokuwa kile alichosimulia kutoka kwa Thaabit peke yake. Kwa ajili hiyo Haafidhw Ibn Hajar amesema juu yake katika ”at-Taqriyb”:

”Anayeaminika na mfanya ´ibaadah. Mtu ambaye ni imara zaidi juu ya Thaabit. Lakini kumbukumbu yake ilibadilika mwishoni mwa uhai wake.”

Hishaam ad-Dastawaa-iy amemukhalifu, inapokuja katika cheni yake ya wapokezi na Hadiyth yenyewe, na akasimulia kutoka kwa Abu Qataadah, kutoka kwa Abu Qilaabah, kutoka kwa Khaalid al-Lajlaaj, kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Abbaas, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Nimemuona Mola wangu (´Azza wa Jall). Akasema: ”Ee Muhammad, ni kipi wanachozozana ulimwengu wa juu?”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Nimemuona Mola wangu katika umbo zuri kabisa.”

Hapa ilikuwa ndotoni, kama yalivyothibitisha mapokezi mengine na kupambanuliwa katika ukaguzi wangu wa ”Kitaab-us-Sunnah” (388, 433 na 469) cha Ibn Abiy ´Aaswim. ad-Dastawaa-iy alikuwa madhubuti zaidi katika kupokea kutoka kwa Qataadah kuliko alivyokuwa Hammaad. Kwa hivyo inavyoonekana ni kwamba hakudhibiti cheni yake ya wapokezi, na pia akahifadhi Hadiyth kwa ufupi. Uhakika ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wangu usingizini, kama ilivyosema hilo waziwazi Hadiyth ya Mu´aadh bin Jabal:

”Niliamka usiku, nikatawadha na nikaswali kile ambacho Allaah ameniandikia kuswali, ambapo nikasinzia sehemu yangu ya kuswalia mpaka nikalala. Tahamaki nikamuona Mola wangu akiwa katika umbo zuri kabisa… ”

Ameipokea Ibn Khuzaymah, uk. 143, na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh, kama nilivyolihakiki katika marejeo yaliyotangulia.

Miongoni mwa mambo yanayotilia nguvu kuwa Hadiyth imefupishwa ni kwamba Ibn Abiy ´Aaswim ameipokea kupitia kwa mwalimu wa Ahmad, kutoka kwa al-Aswad bin ´Aamir: Hammaad bin Salamah ametuhadithia… imekuja mwishoni mwa Hadiyth ”ametaja jambo”. Ziada hii inaonyesha wazi kuwa Hadiyth ina mwendelezo ambao ulifupishwa na mmoja wa wapokezi, dhana yangu kubwa ni kwamba ni Hammaad. Pengine hakuihifadhi, na kwa ajili hiyo, kutokana na amana ya kielimu, alijitosheleza kuiashiria. Ukamilifu uko katika mapokezi mengine, khaswakhaswa katika Hadiyth ya Mu´aadh bin Jabal. al-Bayhaqiy amethibitisha kwamba yale yote yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas juu ya maudhui haya uhakika wa mambo ni kwamba ni masimulizi ya ndoto aliyoona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usingizini. Rejea maneno yake katika ”Kitaab-ul-Asmaa´ was-Swifaat”, uk. 447. Nimemnakili pale pahali palipoashiriwa katika ukaguzi wangu wa ”Kitaab-us-Sunnah” cha Ibn ´Abiy ´Aaswim – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 103-104
  • Imechapishwa: 01/07/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy