Mfungaji hafungui kwa kutumia Siwaak. Bali inapendeza kwake kufanya hivo wakati wa mchana na mwishoni mwa mchana kama ambao hawakufunga. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau kama sio kuwatia uzito ummah wangu basi ningewaamrisha kutumia Siwaak wakati wa kila swalah.”

Wameipokea al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy, Ibn Maajah, Abu Daawuud na Ahmad.

Hili ni lenye kuwahusu wafungaji na wengineo katika nyakati zote. ´Aamir bin Rabiy´ah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara zisizohesabika akitumia Siwaak ilihali amefunga.”

Ameipokea Ahmad, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy[1].

Haitakikani kwa mfungaji kusafisha meno yako kwa dawa ya meno kwa sababu ina ushawishi mkubwa na kuna khatari akameza na mate yake tumboni mwake. Inatosha kutumia Siwaak.

Inafaa kwa mfungaji kufanya mambo yanayompunguzia ukali wa joto na kiu kama vile kujitia baridi kidogo kwa maji na mfano wake. Maalik na Abu Daawuud wamepokea kutoka kwa baadhi ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao wamesema:

“Nilimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa ´Arj (jina la maeneo) akijimiminia maji kichwani mwake ilihali amefunga kutokana na kiu au joto.”[2]

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alilowa nguo yake ambapo akaivaa ilihali amefunga.

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa na jiwe lenye shimo linalofanana na beseni. Wakati wa joto alikuwa anashuka kukaa ndani yake ilikuwa amefunga. Ni kana kwamba – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – lilikuwa limejaa maji.

al-Hasan amesema:

“Hapana vibaya kwa mfungaji kusukutua maji mdomoni na kujitia baridi.”

Athar hii ameitaja al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi pungufu.

Ndugu wapendwa! Jifunzeni dini ya Allaah ili muweze kumwabudu Allaah kwa utambuzi. Kwani hawalingani sawa wale wanaojua na wale wasiojua. Na yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa ufahamu katika dini.

[1] Ameitaja al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu kwa njia ya kuashiria kuwa ni dhaifu (صيغة التمريض). Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy. Haafidhw Ibn Hajar amesema maeneo fulani katika ”Talkhiysw”:

”Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.”

[2] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 110-111
  • Imechapishwa: 05/03/2024