Swali 80: Ni zipi nasaha zako kwa wale wanaosema kuwa nchi hii inaipiga vita dini na kuwakandamiza walinganizi?

Jibu: Saudi Arabia tangu kuanzishwa kwake inainusuru dini na waislamu. Haikusimama isipokuwa juu ya msingi huu. Mpaka hii leo inawasaidia waislamu wote ulimwenguni. Misaada hiyo inaweza kuwa ya kipesa, kujenga vituo vya Kiislamu, misikiti, kuwaagiza walinganizi, kuchapisha vitabu (na khaswa Qur-aan), kufungua taasisi za kielimu na vyuo vikuu vya ki-Shari´ah. Nchi inahukumu kwa kutumia Shari´ah ya Kiislamu na kutenga kitengo cha kujitegemea kinachoamrisha mema na kukemea maovu nchini kote. Yote haya ni dalili ya wazi kabisa juu ya kuunusuru Uislamu na waislamu, jambo ambalo linawachukiza wanafiki, waovu na waasi. Allaah atainusuru dini Yake ijapo watachukia washirikina na watu wenye malengo mabaya[1].

Hatusemi kuwa nchi hii imekamilika kwa kila upande na haina makosa. Kila mmoja anayo makosa. Tunamuomba Allaah aisaidie katika kurekebisha makosa. Ikiwa mzungumzaji mwenyewe atajitazama basi atajiona kuwa na makosa ya kutosha ambayo yatamfanya kuona hayaa kuwazungumzia wengine. Sisi – Allaah akitaka – tunaibainisha haki na hatuna shinikizo kutoka kwa yeyote – na himdi zote njema anastahiki Allaah.

[1] Miongoni mwa neema za Allaah juu yetu ni kwamba hakuna kaburi linaloabudiwa badala ya Allaah. Mambo hayako namna hiyo katika nchi nyenginezo. Imefungua pia vituo vya ulinganizi na miongozo nchini kote. Ndani ya misikiti kuna duara za kielimu kwa ajili ya kuhifadhi Qur-aan. Haitakiwi kupekuapekua kasoro hapa na pale na kupuuza juhudi hizi.

Ama kusema kuwa nchi inawakandamiza walinganizi; ni kweli kwamba nchi inawakandamiza walinganizi wa upotofu na wanaopingana na mfumo wa Salaf. Allaah aijaze kheri kwa hilo! Ni wajibu wa mtawala kutomwacha kila mmoja akazungumza, kwa sababu mifumo na mirengo mbalimbali inaiharibu ´Aqiydah. Mambo yangelikuwa vipi iwapo kila mmoja Suufiyyah, Raafidhwah, Jamaa´at-ut-Tabliygh, al-Ikhwaan al-Muslimuun, wanaharakati wa siasa, Takfiyriyyuun na wengineo wangelikuwa huru kuongea? Je, watu hawa wanataka kukutwa na zile vurugu zinazoendelea katika baadhi ya nchi jirani kwa madai ya uhuru wa maoni na uhuru wa kusema pasi na vigezo vya ki-Shari´ah?

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 205-206
  • Imechapishwa: 22/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy