80. Kutokea Yerusalemu kupanda juu mbinguni

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Mfano kisa cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusafirishwa mbinguni kwa Mola Wake[1], kushuka kwa Malaika kutoka kwa Allaah na kupanda Kwake[2] na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wanapishana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. Wanakusanyika katika swalah ya Fajr na swalah ya ´Aswr. Halafu hupanda wale waliolala kwenu ambapo Mola wenu Anawauliza – ilihali ni mjuzi zaidi kuliko wao: “Mmewaachaje waja Wangu?” Wanasema: “Tumewaacha na huku wanaswali na tumewaendea na huku wanaswali.”[3]

MAELEZO

Dalili nyingine ni safari ya kupandishwa mbinguni. Kupandishwa mbinguni kunaanzia chini na kwenda juu. Alisafiri kuelekea mbinguni akiwa na Jibriyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) kutokea Yerusalemu kwenda mbinguni. Alizivuka mbingu sana na akafika maeneo ambayo Mola alimzungumzisha na kumuongelesha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya yametajwa mwanzoni mwa Suurah ”an-Najm”:

أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ

”Je, mnambishia kuhusu yale aliyoyaona? Kwa hakika amemuona katika uteremko mwingine, kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa, karibu yake kuna bustani ya al-Ma´waa, pindi ulipoufunika mkunazi huo unachokifunika, jicho lake halikukengeuka wala halikupinduka mipaka. Hakika aliona miongoni mwa alama za Mola wake kubwa kabisa.”[4]

Safari ya kupandishwa juu mbinguni imetajwa mwanzoni mwa Suurah ”an-Najm”.

Kuhusu kusafirishwa usiku, ni kule kuchukuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika msikiti Mtakatifu na kwenda katika msikiti wa Aqswaa. Haya yametajwa mwanzoni mwa Suurah ”al-Israa´”:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake [amechukuliwa] ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[5]

Kinacholengwa katika tukio hili ni kutajwa safari ya kupandishwa mbinguni. Kupandishwa mbinguni inakuwa kuelekea kwa juu. Kwa hivyo ikajulisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipandishwa Kwake (´Azza wa Jall).

[1] al-Bukhaariy (346) na Muslim (163).

[2] al-Bukhaariy (6406) na Muslim (2690).

[3] al-Bukhaariy (3223) na Muslim (632).

[4] 53:12-18

[5] 17:1

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 117-118
  • Imechapishwa: 21/08/2024