80. al-Qummiy upotoshaji wake wa kumi na mbili wa Aal ´Imraan

al-Qummiy amesema:

Kuhusiana na maneno Yake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Enyi mlioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara [katika kupambana na imani] na mcheni Allaah ili mpate kufaulu.”[1]

amenieleza baba yangu, kutoka kwa Abu Baswiyr, kutoka kwa Ibn Abiy ´Umayr, kutoka kwa Ibn Miskaan, kutoka kwa Abu ´Abdillaah aliyesema: “Subirini juu ya matatizo na zidisheni kuvuta subira juu ya faradhi na pambaneni juu ya maimamu.”[2]

Aayah inawalenga waumini, lakini Raafidhwah Baatwiniyyah wanayapotosha maneno ya Allaah na kuyapindisha mahala pasipokuwa pake.

Aayah ina maanisha mashaji´isho na kubakia misikitini kwa ajili ya ´ibaadah, jambo ambalo limepokelewa katika Hadiyth nyingi. Maimamu na Raafidhwah wana nini kuhusiana na Aayah na khaswa khaswa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah wake na kipindi cha kushuka Qur-aan? Huoni kuwa watu hawa wanafanya mzaha na kucheza na Qur-aan?

Uongozi wao na yenye kufungamana nayo ni mambo hayana msingi katika Uislamu na si katika malengo yake. Ni katika uzushi tu wa wafuasi wa Ibn Sabaa´. Watu hawa hawajali kumsemea Allaah uongo na kuyapindua maneno kuyaondosha mahala pake stahiki.

[1] 03:200

[2] Tafsiyr al-Qummiy (1/129).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 117-118
  • Imechapishwa: 13/04/2017