Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Zipo Hadiyth nyingi Swahiyh na nzuri ambazo kuhesabika kwake ni kwa tabu kuhusu mada hii.

MAELEZO

Alipomaliza kutaja dalili ndani ya Qur-aan, akabainisha (Rahimahu Allaah) ya kwamba katika Sunnah pia kuna Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinazofahamisha sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta´al). Ima Hadiyth hizo zikawa nzuri au pia Swahiyh.

Sunnah ni Wahy kutoka kwa Allaah na si jambo limezuliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haina maana kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye ameivumbua Sunnah au amejisemea tu yeye mwenyewe. Sunnah ni Wahy kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall):

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekhabarisha katika Hadiyth nyingi kuhusu Allaah kuwa juu na kulingana Kwake, kama itakavyokuja huko mbele.

Sunnah ni Wahy wa pili baada ya Qur-aan. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni. Mcheni Allaah! Hakika Allaah ni mkali wa kuadhibu.”[2]

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا

“Atakayemtii Mtume basi hakika amemtii Allaah na atakayekengeuka, hatukukutuma kuwa mlinzi juu yao.”[3]

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Sema: ”Mtiini Allaah na mtiini Mtume, mkigeukilia basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa; na mkimtii mtaongoka na hapana juu ya Mtume isipokuwa ufikishaji wa wazi.”[4]

Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni hoja ya kukata ubishi kabisa. Sunnah ni Wahy wa pili baada ya Qur-aan. Sunnah inaifasiri Qur-aan, kuiweka wazi, kuifahamisha na kuiweka wazi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaibainisha Qur-aan kupitia Sunnah, kwa sababu Allaah amempa jukumu Mtume Wake kuibainisha Qur-aan hii:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na huenda wakapata kuzingatia.”[5]

Ameibainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ubainifu wa hali ya juu, khaswakhaswa jambo la ´Aqiydah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameibainisha na kuiweka wazi ´Aqiydah kwa uwazi kabisa. Ameuwacha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ummah wake katika njia ya wazi ambayo usiku wake ni kama mchana wake.

[1] 53:3-4

[2] 59:7

[3] 4:80

[4] 24:54

[5] 16:44

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 116-117
  • Imechapishwa: 21/08/2024