78. Dalili juu ya kwamba aliyefikwa na msiba hapewi ujira kwa sababu ya msiba wake

Kuna wanachuoni waliosema kuwa yule aliyefikwa na msiba hapewi thawabu kwa sababu ya msiba wake isipokuwa kwa kule kuwa kwake na subira juu ya msiba huo kwa kutumia hoja ya maneno ya Allaah (Ta´ala):

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.” 39:10

Ibn ´Abdis-Salaam amesema katika “al-Qawaa´id” yake:

“Thawabu zinakuwa kwa kile kitendo cha mja na sio kwa kitendo cha Allaah kwa mtu huyo.”

Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.” 02:156-157

Hii ina maana kwamba ile baraka, rehema na uongofu walioupata kutoka kwa Allaah ni kwa sababu ya kusema kwao:

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

Maneno haya ndio sababu ya kupata yaliyotajwa. Vilevile amesimulia Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) husema: “Ee Malaika wa mauti! Umemchukua mtoto wa mja wangu? Umechukua kipumbazo cha macho yake na matunda ya moyo wake?” Ndipo atajibu: “Ndio.” Allaah aseme: “Alisema nini?” Ajibu: “Amekushukuru na kusema “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” Ndipo Allaah aseme: “Mjengee mja Wangu nyumba Peponi na ipeni jina “Nyumba ya shukurani”.”

Hii ni dalili inayothibitisha kuwa amepata nyumba Peponi kwa sababu ya kumshukuru kwake Allaah na kusema “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea”. Jina la nyumba linatosha.

al-Qaadhwiy ´Iyaadhw ametaja kuwa imepokelewa ya kwamba Ibn Mas´uud amesema:

“Thawabu haziandikwi kwa sababu ya yale maumivu. Yanafuta madhambi peke yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 173
  • Imechapishwa: 17/11/2016