77. Watu wenye furaha zaidi ulimwenguni

Wapi zinaweza kulinganishwa fatwa za Ibn ´Abbaas, tafsiri yake na kunyofoa kwake hukumu kutoka kwenye Maandiko na fatwa na tafsiri ya Abu Hurayrah? Hata hivyo Abu Hurayrah alikuwa ni mwenye kuhifadhi zaidi kuliko yeye; bali yeye ndiye mtu ambaye amehifadhi zaidi katika ummah bila ya ubishi wowote. Akiwasilisha Hadiyth kama alivyoisikia na alikuwa akisoma usiku Hadiyth kwa kurudia. Basi hima yake ilikuwa imeelekezwa katika kuhifadhi na akawasilisha alichokihifadhi kama alivyokisikia. Hima ya Ibn ´Abbaas ilikuwa katika kuelewa na kunyofoa hukumu kutoka kwenye Maandiko, kufungua mito kutoka humo na kutoa hazina zake.

Hali ni hii pia kwa watu waliokuja baada yao wakagawanyika mafungu mawili. Fungu la kwanza wamehifadhi na wanajishughulisha na usahihi wa kuhifadhi na kusilimu Hadiyth kama walivyoisikia bila ya kunyofoa hukumu wala kutoa hukumu zilizofichika ndani ya Maandiko waliyoyahifadhi. Fungu la pili wanatilia umuhimu wa kunyofoa hukumu na kutoa hukumu kutoka katika Maandiko na kuelewa yaliyomo ndani yake. Mfanio wa kundi la kwanza ni kama Abu Zur´ah, Abu Haatim na Ibn Waarah. Kabla yao ni kama Bundaar, Muhammad bin Bashshaar, ´Amr an-Naaqid na ´Abdur-Razzaaq. Kabla yao ni kama Muhammad bin Ja´far Ghundar, Sa´iyd bin Abiy ´Aruubah na wengineo miongoni mwa watu wa hifdhi, usahihi na nidhamu ya kile walichokisikia bila ya ustadi na kuchukua hukumu kutoka katika matamshi ya Maandiko.

Fungu la pili ni kama Maalik, ash-Shaafi´iy, al-Awzaa´iy, Ishaaq, Imaam Ahmad bin Hanbal, al-Bukhaariy na Abu Daawuud, Muhammad bin Naswr al-Marwaziy na wengineo ambao wamekusanya kati ya kunyofoa hukumu na uelewa wa mapokezi.

Mafungu haya mawili ndiyo viumbe wenye furaha zaidi juu ya kile ambacho Allaah amemtuma nacho Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nao ndio wale waliokipokea na wakakipa heshima.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 138-141
  • Imechapishwa: 27/08/2025