77. Dalili kwamba aliyepatwa na msiba analipwa kwa msiba wake

Wanachuoni wametofautiana kiasi kikubwa kama misiba inachangia thawabu au inafuta madhambi. Baadhi ya wanachuoni wamesema kuwa msibiwaji analipwa kwa kila msiba. Kundi lingine la wanachuoni wakasema kuwa halipwi kabisa kwa msiba isipokuwa analipwa kwa ile subira yake kuivumilia. Maoni haya ameyathibitisha Ibn ´Abdis-Salaam katika “al-Qawaa´id” yake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na wanachuoni wengine wamesema kuwa maoni yote mawili ni makosa na kwamba kuna tofauti yenye kuathiri katika suala hili ambayo tutakuja kuitaja baadaye – Allaah akitaka.

Wanachuoni waliosema kuwa msibiwaji analipwa kwa kila msiba wametumia hoja maneno ya Allaah (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ لَا يُصِيبُهُمْ ظَمَأٌ وَلَا نَصَبٌ وَلَا مَخْمَصَةٌ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَطَئُونَ مَوْطِئًا يَغِيظُ الْكُفَّارَ وَلَا يَنَالُونَ مِنْ عَدُوٍّ نَّيْلًا إِلَّا كُتِبَ لَهُم بِهِ عَمَلٌ صَالِحٌ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ

“Hivyo ni kwa kuwa wao haiwasibu kiu, wala machofu, wala njaa kali katika njia ya Allaah, na wala hawakanyagi njia yoyote inayowaghadhibisha makafiri, na wala hawawasibu maadui msiba wowote isipokuwa [yote haya] wanaadikiwa kwayo matendo mema. Hakika Allaah hapotezi ujira wa wafanyao wema.” 09:120

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muislamu hapatwi na kutaabika, uzito, maradhi, huzuni, maudhi, dhiki mpaka ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kwayo.”

al-Bukhaariy amepokea kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote katika watu ambaye watoto wake watatu wanakufa kabla ya kubaleghe isipokuwa Allaah atamwingiza Peponi kwa sababu ya huruma Wake mpana kwao.”

Hadiyth kuhusu mwanamke wa kifafa inathibitisha kuwa kifafa kinafanya mtu kupata thawabu kamilifu zaidi.

Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah aliyesema:

“Kuna mwanamke alikuja na mvulana na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Muombee kwa Allaah! Nimeshazika watatu.” Akasema: “Umeshazika watatu?” Akajibu: “Ndio.” Akasema: “Hakika umejichukulia ngao yenye nguvu kutokamana na Moto.”

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Kukosa thawabu wakati wa msiba ni msiba mkubwa kuliko msiba wenyewe.”

al-Haakim amepokea kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye msiba ni yule mwenye kunyimwa thawabu.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 171-173
  • Imechapishwa: 16/11/2016