Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:
127 – Dini ya Allaah ardhini na mbingu ni moja tu, nayo ni Uislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:
إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ
”Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.”[1]
وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا
”… na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[2]
MAELEZO
Ibn Abiyl-´Izz (Rahimahu Allaah) amesema:
”Uislamu ndio dini ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewawekea katika Shari´ah waja Wake kupitia Mitume Yake. Msingi na tanzu za dini hii ni yale yaliyosimuliwa kutoka kwa Mitume. Iko wazi kwa kiwango cha juu kabisa. Kila mtu mwenye uwezo wa kupambanua, pasi na kujali ni mdogo na mkubwa, msomi na asiyekuwa msomi, mwenye busara na asiyekuwa na busara, anaweza kuingia kwa wepesi kabisa. Vivyo hivyo kwa upesi kabisa mtu anaweza kutoka ndani ya Uislamu kwa kukanusha, kukadhibisha, kupinga, kumkadhibisha Allaah (Ta´ala), kutilia shaka kitu kilichosemwa na Allaah (Ta´ala), kurudisha nyuma kitu kilichoteremshwa, kutilia shaka jambo ambalo si la kutiliwa shaka na mfano wake. Qur-aan na Sunnah vimefahamisha juu ya kudhihiri kwa Uislamu na urahisi wa kujifunza nao. Ilikuwa inaweza kutokea kunakuja ujumbe, unajifunza dini kisha unarejea upesi. Mafunzo yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalikuwa yanaweza kutofautiana kwa kutegemea yule mwanafunzi anayemfunza. Ikiwa mwanafunzi huyo anatokea mbali, kama ujumbe wa Dhwimaam bin Tha´labah an-Najdiy na ´Abdul-Qay, basi anawafunza yale mambo ambayo haifai kutokosa kuyajua. Vilevile alitambua kuwa Uislamu utaenea ulimwenguni na akiwatuma watu maeneo mbalimbali wawafunze yale wanayoyahitaji. Wale waliokuwa wakiishi maeneo ya karibu, walikuwa wanaweza kuja kila wakati, kwa njia ya kwamba wanaweza kuja mara kwa mara na kujifunza hatua kwa hatua, au akajua kuwa tayari amekwishayajua yale mambo ambayo analazimika kuyajua, basi anamjibu muulizaji kutegemea hali na haja yake. Mfano wa hilo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
”Sema: ”Nimemwamini Allaah kisha kuwa na msimamo.”[3]
Kuhusu mwenye kuweka dini isiyokuwa na dalili kutoka kwa Allaah haiwezekani ikawa na misingi yenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Mitume wengineo. Batili inapelekea katika batili kama ambavo haki inapelekea katika haki.”[4]
[1] 3:19
[2] 5:3
[3] Muslim (38), at-Tirmidhiy (2410), Ibn Maajah (3972) na Ahmad (14990).
[4] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 787-788
- Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 108-110
- Imechapishwa: 27/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket