74. Matamshi ya Tashahhud – Tamko la Ibn ´Umar

3- Tashahhud ya Ibn ´Umar. Ibn ´Umar amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

التحيات لله، [و]الصلوات [و]الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume[1]! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah[2] na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”[3]

[1] Ibn ´Umar amesema:

“Niliongeza:

و بركاته

“… na baraka Zake… “

[2] Ibn ´Umar amesema:

“Niliongeza juu yake:

وحده لا شريك له

“… hali ya kuwa yupekee, hana mshirika… “

Nyongeza mbili hizi katika Tashahhud zimethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ibn ´Umar hakuziongeza kutoka kwake mwenyewe. Asingeweza kamwe kufanya kitu kama hicho. Nyongeza mbili hizo alijifunza nazo kutoka kwa Maswahabah wengine waliozisikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaziongeza katika Tashahhud yake aliyoisikia moja kwa moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[3] Abu Daawuuud na ad-Daaraqutwniy ambaye ameisahihisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 141-142
  • Imechapishwa: 30/12/2018