Hivyo basi fungu la mnafiki katika mvua hiyo ni mawingu, ngurumo na radi tu. Hakuweza kujua yaliyoko nyuma yake na hivyo akaingiwa na khofu kutokana na yale waliyojiridhia nayo waumini, akatia shaka katika yale waliyoamini kwa yakini wale waliotambua na akasita katika yale ambayo wanaoona kwa ukweli wameyaepuka. Kwa hiyo macho yake katika mfano wa moto ni kama jicho la popo mchana wa adhuhuri na masikio yake katika mfano wa maji ni kama ya anayekufa kwa sauti ya radi. Imepokelewa ya kwamba baadhi ya wanyama hufa kwa sababu ya kusikia radi. Pale akili hizi, masikio na macho yanapopatana na shubuha za kishaytwaan, mawazo potofu na dhana za uongo, basi huingia ndani yao, husimama humo na kukaa, hujipanua humo na kunenea humo maneno mengi yasiyo na maana na hivyo kujaza masikio na ardhi kwa upuuzi wao na maandiko yao. Ni wengi waliowaitikia hawa, waliowakubali, wanaosimamia wito wao, kuwatetea, kupigana chini ya bendera zao na kuongeza idadi yao!

Kwa ajili ya ukubwa wa balaa lao na madhara yao katika nyoyo kwa maneno yao, Allaah amefichua pazia zao katika Kitabu Chake kwa kiwango cha juu kabisa na akafichua siri zao kwa kiwango cha juu kabisa. Akabainisha alama zao, matendo yao na maneno yao. Allaah (´Azza wa Jall) hakuacha kusema:

وَمِنْهُمْ

”Miongoni mwao… ”

mpaka ikadhihirika hali yao na siri zao zikafunuliwa waziwazi.

Mwanzoni mwa Suurah ”al-Baqarah” Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametaja sifa za waumini, makafiri na wanafiki. Amezitaja sifa za waumini kwa Aayah tatu, sifa za makafiri kwa Aayah mbili na sifa za wanafiki kwa Aayah kadhaa kwa sababu ya wingi wa mtihani kwao na ukubwa wa msiba wa kuchanganyika nao. Kwani wao ni wa ngozi moja ambao wanaonyesha makubaliano na msaada, kinyume na kafiri ambaye adui yake amewekwa wazi kabisa na dhahiri na anakuita uondokane naye na utengana naye.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 130-132
  • Imechapishwa: 26/08/2025