Swali 73: Baadhi ya walinganizi wanaitukana nchi hii na wanazuoni wake na kwamba wanawatuhumu kuwa ni wanazuoni wanaojikombakomba kwa serikali na pia eti hawajui mambo ya kisasa. Sambamba na hilo wanazisifu nchi nyenginezo ambazo zinazotumbukia katika makosa makubwa na walinganizi na wazushi wanaoenda kinyume na mfumo wa Salaf. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Hakuna ninachowatakia waislamu kwa jumla na khaswa wa nchi hii isipokuwa tu kheri na maelewano. Jamii yetu ndio jamii bora inapokuja kwa watawala, wanazuoni na wananchi wake. Hatusemi kuwa ni wakamilifu. Mtu anatakiwa kuwa na inswafu, lakin hatuwezi kuikanusha neema na fadhilah ya Allaah juu yetu. Kwa sababu kufanya hivo itakuwa ni kukufuru neema. Tuko na wanazuoni na watawala walionyooka. Wao sio wajamaa, chama cha Ba´th au madhehebu mengine yanayopingana na Uislamu. ´Aqiydah yao ni ya Tawhiyd na dini yao ni Uislamu. ´Aqiydah yao imesalimika kutokana na shirki. Wanasimamisha adhabu zilizowekwa katika Shari´ah na wanaamrisha mema na kukemea maovu. Wanahukumu kwa Kitabu cha Allaah nchini kote. Mahakama yanahukumu kwa Shari´ah ya Allaah. Ni kweli makosa yapo, lakini kheri ndio nyingi zaidi. Kwa hivyo ni lazima kwetu kuwatakia kheri na kuwaomba kuwafikishwa. Wanatakiwa kunasihiwa kwa siri na kuwafikishia haki. Hili ndio la wajibu kwetu.

Je, tunataka kuisambararisha jamii hii? Je, tunataka jamii hii iingie ndani ya magomvi? Je, tunataka kuvuruga amani ya jamii hii na hivyo watu wasiwe na amani juu ya mali, nyumba na familia zao? Je, tunataka kuondosha neema hii? Mcheni Allaah na mshukuruni Allaah juu ya neema hizi. Msidanganyike na propaganga za kipotofu ambazo zinashawishi mpangilio, zinatafuta makosa na wanazikuza. Wao kazi ni kuona mapungufu ya wengine na hawaoni makosa yao wenyewe.

Tunalazimika kumcha Allaah. Kwani hii ni dini na jukumu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Usiposhukuru juu ya neema inaondoka. Amesema (Subhaanah):

لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ

“Mkishukuru, bila shaka Nitakuzidishieni  na mkikufuru, basi hakika adhabu Yangu ni kali!”[1]

Ilinganishe nchi hii na nchi nyenginezo, ikiwa mko na akili. Linganishe mtaona tofauti. Mnajua nini sababu? Sababu ni kuwa nchi hii iko na ´Aqiydah sahihi, inahukumu Kitabu cha Allaah, kuamrisha mema na kukataza maovu. Hii ni neema kubwa. Waislamu wanaowatakia wengine mema hawazikabili kwa kuzikufuru, kuzipinga na kuzikanusha. Hawatafuti kasoro na makosa na baadaye wakayafanya kuonekana makubwa.

[1] 14:7

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 183-185
  • Imechapishwa: 05/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy