73. Mtenda dhambi kwa mtazamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah

Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Licha ya hivyo wao hawawakufurishi waislamu kwa kutenda maasi na madhambi makubwa, kama wanavyofanya Khawaarij. Bali udugu wa kiimani bado upo pamoja na kuwepo kwa maasi. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala) katika Aayah ya kisasi:

فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ

”Na anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema naye alipe kwa wema.” (02:178)

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَى فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّى تَفِيءَ إِلَى أَمْرِ اللَّهِ فَإِن فَاءتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Na makundi mawili ya waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao, [lakini] mojawapo likikandamiza jengine, basi lipigeni vita lile linalokandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu na fanyeni haki. Hakika Allaah anapenda wafanyao haki. Hakika waumini ni ndugu, basi suluhisheni kati ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.” (49:09-10)

Hawaipingi imani ya muislamu mtenda madhambi moja kwa moja na wala hawasemi kuwa atadumishwa Motoni milele, kama wanavyosema Mu´tazilah. Bali wakati fulani muislamu mtenda madhambi anaingia pia katika imani. Kama ilivyo katika maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَئًا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ

“Atakayemuua muumini kwa kukosea, basi aachilie huru mtumwa muumini…” (04:92)

Na wakati mwingine yawezekana akawa haingii katika imani kamilifu. Kama ilivyo katika maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

”Hakika hapana vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani.” (08:02)

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, na wala hanywi pombe pindi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini, na hapori mwenye kupora pindi anapopora kitu chenye thamani, jambo ambapo linafanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[1]

Tunasemaa kuwa ni muumini mwenye imani pungufu au ni muumini akiwa na imani yake, mtenda dhambi kwa dhambi yake kubwa. Kwa hali hiyo hapewi imani kamilifu na wala haikanushwi moja kwa moja.

MAELEZO

Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni pamoja vilevile na kutompokonya imani muislamu mtenda dhambi ambaye anajinasibisha na Uislamu. Hawaonelei vilevile kuwa atadumishwa Motoni milele. Khawaarij ndio wanampokonya imani yote. Mu´tazilah wanaonelea kuwa atadumishwa Motoni milele. Muislamu mtenda dhambi anaingia katika imani. Kwa mfano maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَئًا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ

“Atakayemuua muumini kwa kukosea, basi aachilie huru mtumwa muumini..”

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli!” (09:119)

Anaingia ndani ya wito huu ambao wanazungumzishwa wale walioamini. Ama sehemu za matapo na sifa hawi mwenye kuingia. Kwa mfano katika maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

”Hakika hapana vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani.”

Vivyo hivyo haingii katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, na wala hanywi pombe pindi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini, na hapori mwenye kupora pindi anapopora kitu chenye thamani, jambo ambapo linafanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[2]

Vilevile dalili nyenginezo mfano wa hizo.

Kwa haya inapata kujulikana ya kwamba muumini mwenye imani kamilifu haingii katika mkumbo wenye kusimangwa. Upande mwingine muumini mwenye imani pungufu anaingia katika mkumbo wenye kusimangwa:

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba… “

Kwa sababu imani yake ni pungufu. Tunapozungumzia waumini wenye imani kamilifu waislamu watenda madhambi wanatoka humo.

Wasifu wa imani ni yule muislamu ambaye anazungumzishwa kutokana na imani yake. Hivyo muislamu mtenda dhambi kuna uwezekano akaingia katika maneno Yake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقُولُوا رَاعِنَا وَقُولُوا انظُرْنَا وَاسْمَعُوا ۗ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ

”Enyi walioamini! Msiseme: ”Tusikilize!” lakini semeni: ”Tuangalie” – na utusikilize; makafiri watapata adhabu iumizayo.” (02:104)

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

“Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.” (03:19)

Vivyo hivyo akaingia katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muislamu ni ndugu yake muislamu.”[2]

Anaingia humu muislamu mtenda dhambi na asiyekuwa mtenda dhambi. Lakini kunapotajwa imani kamilifu yenye kuambatana na sifa, basi muislamu mtenda dhambi haingii humo. Lakini kunapotajwa imani isiyofungamanishwa muislamu mtenda dhambi anaingia humo. Kama ilivyotangulia hapo mbele kwa mfano maneno Yake:

فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ

“Na anayesamehewa na ndugu yake kwa lolote, basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani.” (02:178)

Muuaji ameitwa kuwa ni “ndugu”. Amesema tena:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

“Hakika hapana vyenginevyo waumini ni ndugu.” (49:10)

Wameitwa kuwa ni “ndugu” pamoja na kuwa wamepigana vita.

Kwa kifupi ni kwamba muislamu mtenda dhambi anaingia katika imani isiyofungamanishwa:

فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ

“Na anayesamehewa na ndugu yake kwa lolote, basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani.”

na:

وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَئًا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ

“Atakayemuua muumini kwa kukosea, basi aachilie huru mtumwa muumini…”

Kuna Aayah nyenginezo mfano wa hizi.

Sambamba na hilo haingii katika imani kamilifu ambayo watu wake wamesifiwa. Kwa mfano maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“Hakika hapana vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao, zinajaa khofu wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea. Ambao wanasimamisha swalah na katika yale tuliyowaruzuku hutoa.” (08:02-03)

Vilevile maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba… “

Kutenda kwake dhambi kumefanya akakosa imani kamilifu. Mtu sampuli hii huitwa muislamu, muumini mwenye imani pungufu au pia mtu anaweza kusema kuwa ni muumini kutokana na imani alionayo na ni mtenda dhambi kutokana na dhambi yake kubwa. Hivyo hapewi jina la muumini isiyofungamanishwa na wala anakuwa hakupokonywa nalo. Mtu kama huyu mtu hafai kusema kuwa ni muumini mwenye imani kamilifu kama ambavyo haitakikani vilevile kusema kuwa sio muumini. Isipokuwa ikiwa kama mtu anakusudia kuwa sio muumini mwenye imani kamilifu.

Kwa haya wanaraddiwa Mu´tazilah na Khawaarij na mtu anabaki kuwa ni muumini kwa mujibu wa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah inapokuja katika jambo hili kubwa ambalo wengi wameteleza na kupotea.

[1] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[3] al-Bukhaariy (2442) na Muslim (2580)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 109-110
  • Imechapishwa: 03/11/2024