72. Imani kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah

Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba dini na imani ni kauli na matendo: kauli ya moyo na ulimi na matendo ya moyo na ulimi na viungo vya mwili. Imani inazidi kwa utiifu na inashuka kwa maasi.

MAELEZO

Utafiti huu ni mkubwa katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wanasema kuwa imani ni maneno na vitendo. Maneno ya moyo na ulimi, matendo ya moyo na viungo vya mwili. Haya ndio wanayoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hili ni tofauti na Murji-ah, Mu´tazilah na Khawaarij. Khawaarij wanayakubali haya, lakini wanasema kuwa imani haizidi wala haipungui. Kadhalika Mu´tazilah wanasema kuwa imani haizidi wala haipungui. Wanasema kuhusu imani ima iwepo yote na ikibidi kuondoka inaondoka yote. Kwa ajili hii ndio maana wamemkufurisha mtenda madhambi na kuonelea kuwa ni mwenye kudumishwa Motoni milele. Mu´tazilah pia wameafikiana nao juu ya hilo inapokuja katika hukumu ya Aakhirah na kwamba mtenda madhambi atadumishwa Motoni milele.

Murji-ah wao wameyandosha matendo katika imani na kusema kuwa imani ni kutamka au kusadikisha peke yake. Mapote yote haya yaliyotajwa yamekosea na kupotea kutoka kwenye Njia. Sahihi ni yale waliyomo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambapo wanasema kuwa imani ni maneno na vitendo, maneno ya moyo na ulimi, vitendo vya moyo na viungo vya mwili.

Mfano wa matendo ya moyo ni kama kumpenda Allaah, kumuogopa, kumtakasia nia na kusadikisha. Mfano wa matendo ya viungo vya mwili ni kama kumtaja Allaah, swalah, zakaah, swawm, hajj na kupambana jihaad. Namna hii ndivyo wanavyoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ya kwamba imani ni maneno na matendo, inazidi kwa kufanya mambo ya utiifu na inapungua kwa kufanya mambo ya maasi.

Khawaarij na Mu´tazilah wanaafikiana nao pale wanaposema kuwa imani ni maneno na vitendo. Hata hivyo hawaafikiani nao pale wanaposema kuwa imani inazidi kwa kufanya mambo ya utiifu na inapungua kwa kufanya mambo ya maasi. Sentesi hiyo inawaraddi. Murji-ah wanatoka nje ya jumla hiyo pale wanaposema kuwa imani ni maneno na vitendo. Ni wajibu kwa muumini aamini ´Aqiydah hii na atendee kazi yale inayopelekea.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 106-108
  • Imechapishwa: 03/11/2024