71. Allaah alilingana juu ya ´Arshi katika siku ya saba

71 – Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimshika mkono wake na akasema:

”Ee Abu Hurayrah! Hakika Allaah ameziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ndani ya siku sita. Kisha siku ya saba akalingana juu ya ´Arshi. Akaumba udongo siku ya jumamosi, milima siku ya jumapili, miti siku ya jumatatu, shari siku ya jumanne, nuru siku ya jumatano, wanyama siku ya alkhamisi na Aadam siku ya ijumaa, mwishoni mwa mchana baada ya ´Aswr. Alimuumba kutokana na udongo mwekundu na mweusi mzuri wake na mbaya wake. Ndio maana Allaah akaumba kutokana na Aadam wazuri na wabaya.

Ameipokea an-Nasaa´iy wakati alipokuwa akifasiri Suurah ”as-Sajdah”. al-Akhdhwar bin ´Ajlaan alikuwa madhubuti kwa mujibu wa Ibn Ma´iyn. Abu Haatim ameona kuwa ziandikwe Hadiyth zake ilihali al-´Azdiy ameona kuwa ni mlaini[1]. Hadiyth zake zimesimuliwa na Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah.

[1] Maoni ya al-´Azdiy hayana taathira yoyote, kwa sababu yeye mwenyewe amekosolewa. Kama unavoona mwenyewe amefanywa kuwa madhubuti na Ibn Ma´iyn. Amefanya hivo pia Imaam al-Bukhaariy, an-Nasaa’iy, Ibn Hibbaan na Ibn Shaahiyn, kama ilivyokuja katika “Tahdhiyb-ut-Tahdhiyb”. Kama isingelikuwa kwa ajili ya hukumu ya Ibn Haatim kwamba Hadiyth zake zinaweza kuandikwa, kungelikuwa na maafikiano juu ya umadhubuti wake. Lakini ikiwa tutazingatia kuwa ni kujeruhi kuliko wazi, hayawezi kukubaliwa kwa sababu hayakupambanuliwa, khaswa kwa kuzingatia kwamba ameenda kinyume na maneno ya maimamu wengine ambao wamemfanya kuwa ni madhubuti. Hata hivyo kuna uwezekano wa kuyaoanisha kwa njia ya kwamba akawa ni wa kati na kati kwa mujibu wa Abu Haatim, ikiwa na maana Hadiyth zake angalau kwa uchache ni nzuri. Pengine ndivo alivokuwa akikusudia Haafidhw Ibn Hajar pale aliposema katika ”Taqriyb-ud-Tahdhiyb” ya kwamba ni mkweli. Kwa hivyo wasimulizi waliosalia katika cheni ya wapokezi ni madhubuti. Kwa hiyo cheni ya wapokezi ni nzuri, ingawa si yeye peke yake aliyepokea kuumbwa kwa udongo siku ya jumamosi na kuumbwa kwa viumbe wengine katika yale masiku mengine ya wiki. Muslim (1833) na wengineo wameipokea kupitia njia zingine, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh), kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Baadhi wamefikiri kuwa sehemu ya mwanzo ya Hadiyth inapingana na Aayah ya ”as-Sajdah”. Si sahihi, kama nilivyobainisha katika ”al-Mishkaah” (5735). Ufupisho wa hayo ni kwamba siku saba za Hadiyth sio zile siku sita za ndani ya Qur-aan. Hadiyth inazungumzia kwa upambanuzi zaidi juu ya yale ambayo aliumba ardhini. Kwa msemo mwingine ni kwamba Hadiyth inatoa maelezo zaidi kuliko yale yaliyomo ndani ya Qur-aan. Nilithibitisha uoanishaji huu kabla ya kuona Hadiyth ya al-Akhdhwar, jambo ambalo linatamka wazi kuoanisha kwangu – himdi zote njema ni za Allaah ambaye kwa neema Zake yanatimia yale yote mazuri!

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk. 111-112
  • Imechapishwa: 26/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy