266 – Abur-Rabiy´ ametukhabarisha: Ibn-ul-Mubaarak ametukhabarisha, kutoka kwa ´Utbah bin Abiy Hakiym: ´Umar bin Jaariyah al-Lakhmiy amenihadithia: Abu Umayyah ash-Sha´baaniy amenihadithia:

“Nilikuja kwa Abu Tha’labah al-Khushaniy na kusema: “Ee Abu Tha’labah, unasemaje kuhusu Aayah hii?

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.”[1]

Akajibu: “Naapa kwa Allaah! Mimi mwenyewe nilimuuliza nayo mtu mjuzi; nilimuuliza Mtume wa Allaah na akasema: “Mtaamrishana mema na kukatazana maovu. Pindi mnapoona choyo inayotiiwa, matamanio yanayofuatwa, dunia inayopewa kipaumbele na jinsi kila mmoja anavyopendekeza maoni yake, basi hapo shikamana na nafsi yako na uachane na watu wajinga. Mbele yenu kunakuja masiku ambayo mwenye subira ni kama mfano wa aliyeshika kaa [la moto] na mtendaji mwenye kutenda kama nyinyi analipwa ujira wa wanaume khamsini.”[2]

267 – Ibn-ul-Bazzaar ametukhabarisha: Shabaabah ametukhabarisha, kutoka kwa Yahyaa bin Ismaa´iyl bin Saalim: Nimemsikia ash-Sha´biy akisema:

“Wakati Ibn ´Umar alikuwa katika mali yake, alifikiwa na khabari kwamba al-Husayn bin ‘Aliy alikuwa njiani kuelekea ´Iraaq, ndipo akamuwahi baada ya umbali wa safari ya siku mbili au tatu na akamwambia: “Hakika Jibriyl (‘ alayhis-Salam) alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akampa chaguo kati ya dunia na Aakhirah; akachagua Aakhirah. Hakuitaka dunia. Hakika nyinyi ni sehemu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Naapa kwa Allaah! Hakuna yeyote katika nyinyi atakayeipata.”[3]

268 – Hishaam bin ´Ammaar ametukhabarisha: Yahyaa bin Hamzah ametukhabarisha: Ibn Jaabir ametukhabarisha: Abu ´Abdis-Salaam amenihadithia, kutoka kwa Thawbaan, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Mataifa yanakaribia kukusanyika dhidi yenu kama jinsi walaji wanavyokusanyika kuizunguka sahani.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Je, ni kwa sababu ya uchache wetu kipindi hicho?” Akasema: “Bali nyinyi ni wengi, lakini mtakuwa kama takataka za povu. Allaah ataiondoa khofu katika vifua vya maadui zenu na atatia udhaifu katika nyoyo zenu.” Wakasema: ”Ni nini udhaifu, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kuipenda dunia na kuchukia kwenu kifo.”[4]

269 – Hishaam bin ´Ammaar ametuhadithia mfano wa hayo: Yahyaa bin Hamzah ametukhabarisha: Thawr bin Yaziyd ametukhabarisha, kutoka kwa al-Azhar al-Alhaaniy, kutoka kwa Thawbaan, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

270 – Ahmad bin Muhammad bin Nayzak amenihadithia: Muhammad bin Ja´far ametukhabarisha: ´Abdus-Samad bin Habiyb bin ´Abdillaah al-Azdiy ametukhabarisha, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Shubayl bin ´Awf, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimwambia Thawbaan:

“Unafanya nini, ee Thawbaan, wakati mataifa yatapokusanyika dhidi yenu kama mnavyokusanyika kuizunguka sahani ya chakula ili muweze kukipata?” Thawbaan akasema: “Wazazi wangu watolewe fidia kwa ajili yako, ee Mtume wa Allaah! Je, ni kwa sababu ya uchache wetu?” Akasema: “Mtakuwa wengi, lakini kutawekwa ndani ya nyoyo zenu udhaifu.” Wakasema: ”Ni nini udhaifu, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kuipenda kwenu dunia na kuchukia kwenu kifo.”[5]

[1] 5:105

[2] Abu Daawuud (4341), at-Tirmidhiy (3058), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na ngeni, na Ibn Maajah (4014). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (3058).

[3] Ibn Hibbaan (6968).

[4] Abu Daawuud (4297). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (4297).

[5] Ahmad (8496).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin Abiy ´Aaswim ash-Shaybaaniy (a.f.k. 287)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-uz-Zuhd, uk. 70-72
  • Imechapishwa: 23/07/2025