70. Anayeamini kitu katika Uislamu na kukanusha kingine ni kafiri

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Jibu ni: “Hakuna tofauti kati ya wanachuoni wote, ya kwamba mtu akimsadikisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kitu na akamkadhibisha katika kitu kingine, ni kafiri ambaye hakuingia katika Uislamu. Hali kadhalika [ni kafiri lau] ataamini kitu katika Qur-aan na akapinga kitu kingine, kama mwenye kukubali Tawhiyd na akakadhibisha [kupinga] uwajibu wa swalah, au akakubali Tawhiyd na swalah na akakadhibisha uwajibu wa zakaah, au akakubali Tawhiyd na swalah na akakadhibisha uwajibu wa zakaah, au akakubali yote haya na akakadhibisha swawm, au akakubali yote haya na akakadhibisha hajj. Wakati baadhi ya watu katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakujisalimisha juu ya Hajj, Allah aliteremsha juu yao:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

“Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu.” (03:97)

MAELEZO

Wanazuoni wameafikiana juu ya kwamba mwenye kukufuru na kukadhibisha kitu alichokuja nacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi amekufuru na kukadhibisha vyote. Mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja, basi amewakadhibisha Mitume wote. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَنْ يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَنْ يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَلِكَ سَبِيلًا أُولَئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُهِينًا

“Hakika wale waliomkanusha Allaah na Mtume Wake na wanataka kufarikisha kati ya Allaah na Mtume Wake na wanasema: “Tunaamini baadhi na tunawakanusha baadhi”; na wanataka kuchukua njia iliyo baina ya hayo – hao ndio makafiri wa kweli; na Tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.” (04:150-151)

Vilevile amesema (Ta´ala) juu ya wana wa israaiyl:

أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍۚ فَمَا جَزَاءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰ أَشَدِّ الْعَذَابِ ۗوَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ

“Je, mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakanusha baadhi yake? Basi hapana malipo ya anayefanya hayo miongoni mwenu isipokuwa utwevu katika maisha ya duniani, na Siku ya Qiyaamah watapelekwa kwenye adhabu kali zaidi, na Allaah si Mwenye kughafilika kwa myatendayo.” (02:85)

Halafu mtunzi akaleta baadhi ya mifano:

1 –  Swalah. Anayethibitisha Tawhiyd na akapinga uwajibu wa swalah ni kafiri.

2 – Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… au akakubali Tawhiyd na swalah na akakadhibisha uwajibu wa zakaah… “

Huu ni mfano wa pili. Anayekiri Tawhiyd na swalah akakanusha uwajibu wa zakaah, ni kafiri.

3 – Mwenye kukubali uwajibu wa yaliyotangulia na akakanusha uwajibu wa kufunga, ni kafiri.

4 – Mwenye kuthibitisha yaliyotangulia yote na akakanusha uwajibu wa Hajj, ni kafiri. Mtunzi (Rahimahu Allaah) akatumia dalili maneno Yake (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

“Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu.” (03:97)

Udhahiri ni kuwa hii ndio sababu ya kuteremka kwa Aayah hii. Hata hivyo sitambui dalili ya hayo aliyoyataja Shaykh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 25/11/2023