Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

121 – Hatumfadhilishi yeyote katika mawalii juu ya yeyote katika Manabii. Tunasema kuwa Nabii mmoja ni bora kuliko mawalii wote.

MAELEZO

Ibn Abiyl-´Izz amesema:

”Shaykh (Rahimahu Allaah) anaashiria kuwaraddi wakanamungu na wajinga wa Suufiyyah. Vinginevyo watu wenye msimamo wanausia kufata elimu na Shari´ah. Allaah amewawajibishia Mitume wote kuwafuata Mitume. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah.”[1]

Wengi katika watu hawa wanafikiria kuwa, kwa uongozi wao, kujipinda kwao katika ´ibaadah na malezi ya kiroho, wanaweza kufikia yale waliyofikia Mitume pasi na kufuata njia yao. Miongoni mwao wengine hufikiria kuwa wamekuwa wabora kuliko Mitume. Wengine wakadai kuwa Mitume na Manabii huchukua elimu yao kutoka kwa yule walii wa mwisho. Wengine wakadai kuwa wao ndio mawalii wa mwisho. Uhakika wa mambo elimu hiyo si chochote isipokuwa ule usemi wa Fir´awn, kwamba uwepo huu wenye kushuhudiwa ni wajibu kwa nafsi yake na hauna ambaye kauumba ambaye ametengana nao. Hata hivyo huyu anasema kuwa yeye mwenyewe ndiye Allaah ilihali Fir´awn alipinga uwepo wa Allaah kikamilifu. Lakini Fir´awn kwa ndani alikuwa ni mwenye kumtambua Allaah zaidi kuliko wao, kwa sababu alikuwa akimthibitisha Muumba ilihali hawa wanafikiria kuwa uwepo uliyoumbwa ni ule uwepo uliyoumba. Hiyo ndio ´Aqiydah ya Ibn ´Arabiy na watu mfano wake. Wakati alipoona kuwa Shari´ah ilio dhahiri hakuna njia ya kuibadilisha, ndipo akasema kuwa utume umemalizwa lakini uwalii haukumalizwa. Aidha akadai juu ya uwalii mambo ambayo ni makubwa zaidi kuliko mambo ya utume, yanayokuwa kwa Mitume na Manabii na kwamba Mitume wananufaika kutoka kwa mawalii. Kama alivosema mwenyewe:

Nafasi ya unabii iko katika utume na iko

juu kidogo kuliko ya Mitume lakini chini ya walii[2]

Huku ni kuipindua Shari´ah. Ukweli wa mambo ni kwamba kila muumini na mwenye kumcha Allaah ni walii.  Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha.”[3]

Kama tulivosema kuzindua hapo kabla ni kwamba unabii ni jambo maalum zaidi kuliko uwalii na ujumbe ni jambo maalum zaidi kuliko unabii.”[4]

[1] 4:64

[2] Tazama ”al-Futuwhaat al-Makkiyyah” (2/252) ya Ibn ´Arabiy.

[3] 10:62-63

[4] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 742-744

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: l-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 104-106
  • Imechapishwa: 20/10/2024