70. Kubaki Minaa baada ya kutoka katika Ihraam

Kisha hurudi Minaa ambapo ndipo mahali pekee anapotakiwa kutumia nyusiku zake.

Kisha hurusha vijiwe kwenye kiguzo baada ya jua kupinduka katika siku zake, ambapo kila kiguzo kitarushiwa vijiwe saba. Huanzia nguzo ya kwanza, huelekea Qiblah na hulirushia kwa vijiwe saba kama alivyorusha kwenye nguzo ya ´Aqabah. Kisha husogea mbele na kusimama hapo na kumuomba Allaah. Kisha huenda kwenye nguzo ya kati na kurusha vijiwe vivyo hivyo. Kisha hurusha vijiwe kwenye nguzo ya ´Aqabah na hasimami hapo. Kisha siku ya pili hurusha vijiwe kwa kufanya vivyo hivyo.

Ikiwa anataka kuharakisha na kuondoka kwenda nyumbani baada ya siku mbili, basi hutoka kabla ya jua kuzama. Ikiwa jua litazama akiwa Minaa, inakuwa wajibu kwake kulala Minaa na kurusha vijiwe siku inayofuata.

Ikiwa ni mwenye kufanya Hajj ya Tamattu´ au Hajj ya Qiraan, basi Hajj yake na ´Umrah yake huwa zimekamilika.

Ikiwa ni mwenye kufanya Hajj ya Ifraad, basi hutoka kwenda Tan´iym na huingia katika Ihraam kwa ajili ya ´Umrah kutoka hapo. Kisha huenda Makkah, akafanya Twawaaf na Sa´y, kisha hunyoa au hupunguza nywele. Ikiwa hana nywele, basi inapendekezwa kupitisha wembe juu ya kichwa chake. Hapo Hajj yake na ´Umrah yake huwa zimekamilika.

Hakuna ziada katika matendo ya mwenye kufanya Hajj ya Qiraan kuliko matendo ya mwenye kufanya Hajj ya Ifraad, isipokuwa kwamba yeye pamoja na mwenye kufanya Hajj ya Tamattu´ wanawajibika kuchinja mnyama wa Hadiy. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِذَا أَمِنتُمْ فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ ۚ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ ۗ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ

”Mtakapopata amani, basi mwenye kufanya Tamattu´ kwa kutekeleza ‘Umrah kwanza kisha Hajj, basi achinje mnyama aliye mwepesi. Na asiyepata, basi afunge siku tatu katika Hajj na saba mtakaporejea – hizo ni kumi kamili.”[1]

[1] 02:196

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 11/11/2026