1 – Mutwarrif bin ´Abdillaah amesema:

“Nilimsikia Maalik bin Anas akisema alipomsikia bwana mmoja akikataa Hadiyth za sifa: “´Umar bin ´Abdil-Aziyz amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na watawala baada yake wameweka Shari´ah mbalimbali. Yule mwenye kuzifanyia kazi anathibitisha Kitabu cha Allaah, kukamilisha kumtii Allaah na kuifanyia kazi dini ya Allaah kwa nguvu. Hakuna kiumbe yeyote awezaye kuzibadilisha wala kuzigeuza wala kutazama chochote kinachopingana nazo. Anayechagua kuongozwa basi huyo ndiye kaongozwa na anayetafuta nusura kupitia kwazo basi ni mwenye kupewa nusura. Na yule mwenye kuziacha basi amefuata njia ya wasiokuwa waumini, Allaah atamwacha kuelekea kule alikoelekea na atamwingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”

2 – Ishaq bin ´Iysaa amesimulia kwamba Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

“Je, tuyaache yale ambayo Jibriyl amemteremshia nayo Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kila pale ambapo anakuja mtu ambaye anajadili vizuri kuliko mwengine?”[1]

3 – Abu Thawr amesimulia kuwa amemsikia ash-Shaafi’iy akisema:

“Alikuwa Maalik anapojiliwa na baadhi ya watu wa matamanio husema: “Kuhusu mimi, niko kwenye ubainifu wa dini yangu. Kuhusu wewe, ni mwenye shaka. Hivyo basi, nenda kwa mwenye shaka mfano wako uvutane naye.”

4 – Ibn Wahb amesimulia kwamba Maalik amesema:

“Watu siku ya Qiyaamah watamtazama Allaah (‘Azza wa Jall) kwa macho yao.”

5 – al-Qaadhwiy ´Iyaadhw amesimulia kuwa Ibn Ma´n amesema:

“Siku moja Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah) alinishika mkono na akaenda msikitini. Alipokuwa njiani mtu mmoja aitwaye Abul-Juwayriyah akamuwahi. Bwana huyo alikuwa akituhumiwa kuwa na madhehebu ya Murji-ah. Akasema: “Nisikilize.” Akasema: ”Jihadhari nisije kushuhudia dhidi yako.” Bwana yule akasema: “Naapa kwa Allaah! Hakuna ninachotaka isipokuwa haki tu. Ikiwa umepatia, basi unasema kusema.” Maalik akasema: “Itakuweje ukinishinda?” Bwana yule akajibu: “Itabidi unifuate.” Maalik akasema: “Na vipi ikiwa nitakushinda?” Bwana yule akasema: ”Itabidi nikufuate.” Maalik akasema: “Itakuweje akija mtu mwingine na kunishinda mimi na wewe?” Bwana yule akasema: “Itabidi tumfuate.” Ndipo Maalik akasema: “Allaah (‘Azza wa Jall) amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na dini moja na nakuona unatoka katika dini moja na kwenda katika dini nyingine.”

6 – Maalik amesema:

“Mijadala ya kidini huleta mabishano, ikazima nuru ya elimu moyoni na kuufanya kuwa mgumu na ikaleta kinyongo.”

[1] Twabaqaat-ul-Hanaabilah (2/156).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 15-17
  • Imechapishwa: 27/11/2025