Swali 69: Je, Ashaa´irah, Mu´tazilah na wengine walio na ´Aqiydah kama wao wanakufurishwa? Je, inafaa kusoma ´Aqiydah kwao, Fiqh na tafsiri ya Qur-aan pindi mtu anapojua ni wapi wamekosea?

Jibu: Hakufuru isipokuwa ambaye ameitambua haki na akafanya ukaidi. Kuhusu ambaye anaenda kinyume na haki kwa sababu ya kupindisha maana au ujinga, huyu hakufurishwi. Bali mtu huyo anatiwa katika makosa na upotevu. Ambaye atapindisha maana na akadhani kuwa tafsiri hiyo ni haki, anawafuata kichwa mchunga wengine hali ya kudhani kuwa wamepatia au amefanya hivo kwa ujinga, watu sampuli zote hizi hawakufurishwi. Lakini wanatiwa upotofuni.

Kuhusu kusoma kwao katika maudhui mengine wanayoyajua vizuri yasiyokuwa ´Aqiydah, hapana neno. Mfano wa maudhui zinazoweza kusomwa kwao ni Fiqh, sarufi na somo la Hadiyth. Hapana vibaya kufanya hivo kwa sharti wasiwe wenye kudhihirisha Bid´ah zao. Lakini wakipatikana wengine ambao ni bora kuliko wao basi italazimika kusoma kwa hao ambao ni bora kuliko wao. Lakini mtu asipopata wengine katika mfano wa maudhui kama hayo, kama vile Fiqh na kiarabu, hapana vibaya kusoma kwao masomo hayo. Kuhusu ´Aqiydah haisomwi isipokuwa kutoka kwa wale wenye ´Aqiydah sahihi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 176
  • Imechapishwa: 01/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy