156 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapoona mvua husema:

اللّهُمَّ صَيِّـباً نافِـعاً

“Ee Allaah! Iteremshe kwa wingi na iwe yenye manufaa.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy.

157 – Zayd bin Khaalid al-Juhaniy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituswalisha swalah ya Fajr Hudaybiyah baada ya mvua iliyonyesha usiku. Alipomaliza kuswali akawaelekea watu na akasema: “Je, mnajua nini Kasema Mola wenu?” Wakasema: “Allaah na Mtume wake ndio wanajua zaidi.” Akasema: “Katika asubuhi hii kuna baadhi ya waja Wangu wamepambaukia wakiwa ni wenye kuniamini na wengine wamekufuru. Ama yule aliyesema kwamba: “Tumenyeshewa mvua kwa fadhila na rehema ya Allaah”, basi huyo ndiye aliyeniamini Mimi na amekufuru sayari. Ama yule aliyesema ya kwamba tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani, basi huyo amenikufuru Mimi na ameamini sayari.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

MAELEZO

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah wakati mtu anapoona mvua aseme:

اللّهُمَّ صَيِّـباً نافِـعاً

“Ee Allaah! Iteremshe kwa wingi na iwe yenye manufaa.”

Kwa maana ya kwamba unamuomba Allaah aifanye kuwa ni yenye kunyesha kwa wingi na yenye manufaa. Imekuja katika tamko jengine kwamba amesema:

مطرنا بفضل الله ورحمته

“Tumepewa mvua kwa fadhilah na rehema za Allaah.”

Hii ndio imani. Kuinasibisha mvua kwa Allaah ni katika imani. Na kuinasibisha katika sayari ni katika kufuru.

Akisema:

”Tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani.”

Jambo hili linahitaji upambanuzi:

1 – Akisema hivo hali ya kuamini kuwa nyota zina taathira katika kuteremsha mvua ni shirki kubwa, kama ilivyokuwa kipindi kabla ya kuja Uislamu. Walikuwa wakifanya kuwa nyota zina taathira katika ulimwengu. Ulimwengu huu unaendeshwa na Allaah na hauna mwendashaji mwengine pamoja Naye.

2 – Lakini akiona kuwa nyota ni sababu tu na haina taathira yoyote ni shirki ndogo. Kwa sababu amefanya sababu kitu ambacho Allaah hakukifanya kuwa ni sababu.

3 – Lakini akisema:

مطرنا في نجم كذا

“Tumenyeshewa mvua kwa ajili ya sayari fulani.”

ni jambo linalofaa. Kwa sababu ameeleza kuhusu wakati.

[1] al-Bukhaariy (1032).

[2] al-Bukhaariy (846) na Muslim (71).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 148-149
  • Imechapishwa: 16/11/2025