Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Licha ya hivo Amewaamrisha waja kumtii Yeye na kuwatii Mitume Yake na akawakataza kumuasi. Naye (Subhaanah) anawapenda wachaji Allaah, wenye kufanya wema na waadilifu. Yuko radhi na wale walioamini na kufanya mema. Hawapendi makafiri na wala hawaridhii wenye kufanya maasi. Na wala haamrishi machafu. Haridhii kutoka kwa waja Wake ukafiri na wala hapendi ufisadi.
Waja ndio wenye kutenda kikweli na Allaah ndiye ameumba matendo yao. Mja ndiye muumini na kafiri, mchaji Allaah na mtena dhambi, mwenye kuswali na mwenye kufunga. Waja wana uwezo na matakwa katika kufanya kwao matendo yao. Allaah amewaumba na ndiye ameumba pia uwezo wao na matakwa yao. Kama alivyosema (Ta´ala):
لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
”Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke. Na hamtotaka isipokuwa atakaye Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:28-29)
MAELEZO
Waja ni wenye kutenda kihakika. Matendo wanayofanya yananasibishwa kwao. Mja ndiye mwenye kuswali, mwenye kufunga, mwenye kuhiji, mwenye kuzini, mwenye kuiba, yeye ndiye mwenye kuuza na kununua, mwenye kuoa na kutaliki. Allaah (Subhaanah) ndiye amewaumba na akaumba vilevile matendo yao. Amesema (Ta´ala):
وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ
“Na hali Allaah amekuumbeni na yale mnayoyatenda.” (37:96)
Hakika Allaah (Subhaanah) anawapenda wachaji Allaah, watenda wema na waadilifu. Hawi radhi na watenda dhambi, hawapendi makafiri, haridhii juu ya waja wake kufuru na hapendi ufisadi. Anapenda kheri na watu wake, anachukizwa na shari na watu wake. Yeye anapenda imani na uchaji Allaah na wakati huohuo anachukia ufisadi, kufuru na upotevu. Kila mja ni mwenye kusahilishiwa kwa yale aliyoumbwa kwa ajili yake. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walisema:
“Ee Mtume wa Allaah! Yale tunayofanya yamekwishapangwa au hayajapangwa?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Yamekwishapangwa.” Maswahabah wakasema: “Si tutegemee basi tuliyoandikiwa na tuache kutenda?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Fanyeni matendo! Kwani hakika kila mmoja ni mwenye kufanyiwa wepesi juu ya kile alichoumbiwa.”[1]
[1] al-Bukhaariy (4949) na Muslim (2647).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 102-103
- Imechapishwa: 03/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket