Tambua kwamba makundi miongoni mwa Salaf walikuwa wakiomba kwa wenye kusoma kwa sauti nzuri wasome nao wakisikiliza. Hili limeafikiwa kuwa linapendekezwa. Isitoshe ni desturi ya watu wema, wenye kujitahidi katika ´ibaadah na waja wema wa Allaah. Kitendo hicho ni Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwani imesihi kutoka kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliniambia: “Nisomee Qur-aan.” Nikasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Nikusomee na juu yako imeteremshwa?” Akasema: “Hakika napenda kuisikia kutoka kwa mwingine.” Nikamsomea Suurah ”an-Nisaa´” mpaka nilipofika katika Aayah:

فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ شَهِيدًا

”Basi itakuwaje [siku ambayo] Tutakapoleta kutoka kila Ummah shahidi na tukakuleta wewe pia kuwa shahidi juu ya hawa.”[1]

akasema: “Inatosha sasa.” Nikamgeukia ambapo nikakuta macho yake yanatiririka machozi.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

ad-Daarimiy na wengine wamepokea kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akimwambia Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Tukumbushe Mola wetu.”

Naye alikuwa akisoma Qur-aan mbele yake[3].

Masimulizi katika hili ni mengi na yenye kutambulika. Makundi ya waja wema wamefariki kwa sababu ya kisomo cha waliowaomba wawasomee – na Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

[1] 4:41

[2] al-Bukhaariy (5050) na Muslim (800).

[3] ad-Daarimiy (3493 och 3496).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 26/11/2026