68. Dalili za waziwazi na za dhahiri kuhusu ujuu wa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Mambo yakishakuwa hivo basi Qur-aan kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake, Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake na maneno ya Maswahabah na wanafunzi zao na maneno ya maimamu wengine yamejaa mambo ambayo ima ni dalili ya wazi au ya dhahiri ya kwamba Allaah (Subhaanah) ndiye Aliye juu kabisa, yuko juu ya kila kitu, na kwamba yuko juu ya ´Arshi na kwamba yuko juu ya mbingu.

MAELEZO

Qur-aan imejaa dalili ambazo ziko wazi na dhahiri kuhusu majina na sifa za Allaah. Dalili ya wazi ni ile ambayo haifahamiki kwa njia isipokuwa moja tu. Dalili ya dhahiri ni ile ambayo inaweza kufahamika njia mbili ambapo moja wapo ni yenye nguvu zaidi kuliko nyingine na kwa ajili hiyo itabaki kama inavyodhihiri mpaka kuthibiti dalili kinyume chake. Dalili ya waziwazi inatakiwa kutendewa kazi na hakuna nafasi ya kuiacha. Dalili ya dhahiri inabakia kama ilivyo mpaka kuthibiti dalili inayoigeuza kutoka katika udhahiri wake na kwenda katika maana nyingine ambayo hapo ndipo itachukuliwa.

Qur-aan imejaa ya kwamba Allaah ndiye Aliye juu na Mtukufu kabisa. Amesema (Ta´ala):

وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

”Naye yujuu kabisa, Ametukuka.”[1]

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى

“Tukuza jina la Mola wako Aliye juu!”[2]

Amejisifu Mwenyewe kuwa Yuko juu na kwamba ndiye Mtukufu kabisa. Yuko (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya viumbe Wake kwa dhati Yake, hadhi na nguvu:

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ

“Naye hapingiki Aliye Mkuu kabisa juu ya waja Wake.”[3]

Ujuu umegawanyika katika maana tatu:

1 – Ujuu wa dhati.

2 – Ujuu wa hadhi.

3 – Ujuu wa nguvu.

Watu wa haki wanamthibitishia Allaah aina zote hizi za ujuu, lakini wapotofu wanathibitisha ujuu wa hadhi na nguvu na wanapinga ujuu wa dhati.

[1] 2:255

[2] 87:1

[3] 6:18

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 106-107
  • Imechapishwa: 18/08/2024