67. Ni ipi hukumu ya anayempenda mwanachuoni mapenzi makubwa kiasi kwamba hataki kusikia mtu anamkosoa?

Swali 67: Ni ipi hukumu ya anayempenda mwanachuoni au mlinganizi mapenzi makubwa, kwamba hataki kusikia mtu anamkosoa na kwamba anayakubali maneno yake ijapo yatakuwa yanapingana na dalili? Hoja yao ni kuwa mwanachuoni huyu ni mjuzi zaidi wa dalili kuliko wao?

Jibu: Huu ni ushabiki, unaosimangwa na usiojuzu[1]. Sisi tunawapenda wanazuoni na walinganizi wanaolingania kwa Allaah (´Azza wa Jall), lakini anapokosea mmoja katika wao basi sisi tunabainisha haki kwa dalili. Hilo halipunguzi mapenzi ya yule aliyeraddiwa wala hadhi yake. Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hakuna yeyote katika sisi isipokuwa anaraddi na kuraddiwa – isipokuwa mtu mwenye kaburi hili.”[2]

Bi maana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Sisi tunapowaraddi baadhi ya wanazuoni na baadhi ya watu watukufu, hiyo haina maana kuwa tunawachukia au tunawatia upungufu. Isipokuwa tunabainisha jambo la sawa. Kwa ajili hiyo baadhi ya wamesema baadhi ya wanazuoni walipokosea baadhi ya marafiki zao:

”Tunawapenda, lakini haki ni yenye kupendeza zaidi kwetu.”

Huu ndio mfumo sahihi. Usifahamu kwamba kuwaraddi baadhi ya wanazuoni katika masuala waliyokosea ni kuwatia upungufu au kuwachukia. Wanazuoni daima ni wenye kuraddiana wao kwa wao ilihali ni ndugu wanaopendana.

Haijuzu kwetu kuchukua kila kinachosemwa na mtu, ni mamoja amepatia au amekosea. Huo ndio ushabiki. Ambaye yanachukuliwa maneno yake yote bila kurudishwa nyuma kitu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye anafikisha kutoka kwa Allaah na wala hazungumzi kwa matamanio yake. Kuhusu wengine wanaweza kupatia na wanaweza kukosea, ingawa watakuwa ni watu bora kabisa. Hakuna yeyote aliyesalimika na kukosea isipokuwa tu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni lazima tulitambue hili. Hatufichi kosa kwa sababu ya kuwapenda watu. Bali ni lazima kwetu kuyabainisha makosa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: ”Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wao wa kawaida.”

Kubainisha kosa ni katika kuwatakia mema watu wote ilihali kuficha kunapingana na kutakia mema.

[1] Muhammad Sultwaan al-Khajandiy amesema:

”´Aliy al-Qaariy al-Hanafiy amesema:

“Sio wajibu kwa yeyote katika Ummah huu kuwa Hanafiy, Maalikiy, Shaafi´iy au Hanbaliy. Lililo la wajibu kwa wale ambao sio wasomi, ni kuwauliza wanazuoni – na miongoni mwao kunaingia maimamu wane. Ndio maana kumesemwa:

“Yule mwenye kumuuliza mwanachuoni, atakutana na Allaah hali ya kuwa ni mwenye kuokolewa.”

Kila yule ambaye ´ibaadah ni wajibu juu yake ameamrishwa kumfuata kiongozi wa Mitume, bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” (Hal-il-Muslim Mulzam bi Ittibaa´ Madhhab Mu´ayyan min-al-Madhaahib al-Arba´ah?, uk. 58)

Mfano wa hayo yamesemwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah), kitu ambacho kimeshatangulia. Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Waislamu wameafikiana juu ya kwamba yule atakayebainikiwa na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi haifai kwake kuiacha kwa ajili ya maoni ya mtu mwengine.”  (I´laam-ul-Muwaqqi´iyn (2/361) ya Ibn-ul-Qayyim)

[2] Ibn ´Abdil-Haadiy ameisahihisha katika ”Irshaad-us-Saalik” (1/227). Ibn ´Abdil-Barr ameipokea katika ”al-Jaamiy´” (2/91) na Ibn Hazm katika ”Usuwl-ul-Ahkaam” (6/145) kutoka kwa al-Hakam bin ´Utaybah na Mujaahid.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 173-175
  • Imechapishwa: 01/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy