Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Kundi lililookoka, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanaamini makadirio ya kheri na ya shari yake.
Kuamini makadirio kumegawanyika katika daraja mbili na kila daraja ina mambo mawaili.
1 – Kuamini ya kwamba Allaah (Ta´ala) aliyajua kwa elimu Yake ya milele – ambayo anasifiwa nayo milele na daima – ambayo viumbe watafanya. Vlevile akajua hali zao zote kuhusiana na utiifu, maasi, riziki na muda wao wa kueshi. Kisha Allaah akayaandika makadirio ya viumbe katika Ubao uliohifadhiwa. Kitu cha kwanza aichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika yatayokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.”[1]
Yaliyomfika mtu hayakuwa ni yenye kumkosa, na yaliyomkosa hayakuwa ni yenye kumpata. [Wino wa] kalamu umekauka na sahifu zimefungwa. Amesema (Ta´ala):
أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ
”Je, huelewi kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo ndani ya Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (22:70)
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ
”Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo ndani ya Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (57:22)
Makadirio haya yanaenda sambamba kabisa na ujuzi Wake (Subhaanah). Ameandika kwenye Ubao uliohifadhiwa atakayo. Pindi anapoumba kipomoko, kabla ya kukipulizia roho, hukitumia Malaika na hukiamrisha kuandikwe maneno mane. riziki yake, muda wake wa kueshi, matendo yake na kama atakuwa na mla khasara au mwenye furaha. Makadirio haya walikuwa wakiyakanusha Qadariyyah waliochupa mipaka hapo kale. Hii leo ni wachache wanaoyakanusha.
MAELEZO
Utafiti huu ni miongoni mwa tafiti zenye faida zaidi na zenye kujumuisha. Ni tafiti yenye faida kubwa kuhusiana na makadirio. Mtunzi (Rahimahu Allaah) ameifanyia utafiti kwa kina na kuiweka wazi kama alivyofanya hivyo pia ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim katika kitabu “Shifaa´-ul-´Aliyl”.
Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na sifa za kundi lililookoka ni pamoja na kuamini makadirio ya kheri na ya shari. Kundi lililookoka linaamini makadirio ya kheri na ya shari kwa sura zake zote.
Kuna daraja mbili za kuamini makadirio na kila daraja ina mambo mawili. Kuamini makadirio ndani yake kunahitajia mambo manne ambayo yanaitwa “ngazi nne”. Mwenye kuyakamilisha basi amekamilisha kuamini makadirio.
Ngazi ya kwanza: Ujuzi. Mtu aamini ya kwamba Allaah aliyajua mambo yote.
Ngazi ya pili: Uandishi.
Ngazi ya tatu: Utashi. Anayotaka Allaah, huwa. Na asiyotaka hayawi.
Ngazi ya nne: Uumbaji. Mtu aamini ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji wa kila kitu na kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye ameumba kila kitu. Hana mshirika katika kuumba na kuyaendesha mambo. Hizi ndio ngazi za makadirio. Ni ngazi nne. Mtu aamini ujuzi wa Allah juu ya mambo na kwamba ujuzi Wake umeyazunguka mambo yote. Amesema (Ta´ala):
إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
“Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.” (08:75)
لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا
”… ili mjue kwamba Allaah juu ya jambo ni Muweza na kwamba Allaah amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi.” (65:12)
Huu ni ujuzi Wake wa milele. Kwa msemo mwingine hakuacha hata siku moja kusifika na elimu hii. Elimu yake haifichikani na chochote:
وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ
“Na hushughuliki katika jambo lolote na wala husomi humo chochote katika Qur-aan, na wala hamtendi ‘amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo.” (10:61)
Mambo yote yaliyopo duniani na Aakhirah ni yenye kujulikana Kwake. Hakuna kinachofichikana Kwake (Jalla wa ´Alaa).
Kadhalika mambo haya yameandikwa. Pamoja na kuwa aliyajua akayaandika vilevile. Amesema (Ta´ala):
أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ
”Je, huelewi kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo ndani ya Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ
”Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo ndani ya Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Allaah amekadiria makadirio ya viumbe kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu khamsini na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[2]
Ameandika kila kitu kwenye Ubao uliohifadhiwa. Kalamu iliandika kila kitu kitachokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah. Kwa hiyo daraja ya kwanza imekusanya vipengele viwili: ujuzi na uandishi.
[1] Ahmad (5/317), Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (1/48).
[2]Muslim (2653).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 99-102
- Imechapishwa: 03/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)