67. Dalili ya nguzo za Uislamu, imani na ihsaan

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili kutoka katika Sunnah ni Hadiyth ya Jibriyl inayojulikana iliyopokelewa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Siku moja tulipokuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutokea  mtu ambaye  nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana. Hakuwa na alama  ya kuonesha kuwa ni msafiri na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na mago yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake.” Akasema: “Ee Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu!” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamab Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji ukiweza.”  Akasema: “Umesema kweli.” Tukashangazwa kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha. Kisha akasema: “Nieleze kuhusu imani!”  Akasema: “Ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Mwisho na  kuamini Qadar; kheri na shari yake.” Akasema: “Umesema kweli!” Akasema: “Nieleze kuhusu Ihsaan!”  Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona.”  Akasema: “Nieleze kuhusu Qiyaamah.”  Akasema: “Muulizwaji si mjuzi  kama asivyo vilevile muulizaji.” Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” Akasema: “Kijakazi kumzaa bibi yake na utaona wachunga wanatembea peku, uchi na mafukara wakishindana kujenga majumba marefu.” Amesema: “Kisha akaondoka na tukatulia muda mrefu. Halafu akasema (Swallla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ee ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Nikajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.”  Akasema Mtume: “Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amekuja kuwafundisha Dini yenu.”

MAELEZO

Imepokelewa na Muslim. Inapatikana katika Kitabu kuhusu Iymaan katika mlango “al-Iymaan wal-Islaam”. Tumeshatangulia kufafanua sehemu kubwa ya Hadiyth hii. Pia tumeifafanua katika “Majmuu´ al-Fataawaa war-Rasaa-il”, 3/143.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 121
  • Imechapishwa: 03/06/2020