Allaah (´Azza wa Jall) amepiga mfano wa nuru hii, mahali pake, mbebaji wake na chanzo chake kwa niche, nayo ni shimo katika ukuta. Nayo ni mfano wa kifua. Katika niche hiyo kuna kioo miongoni mwa vioo safi kabisa hata ikafanana na nyota yenye kung’aa sana kwa weupe na usafi wake. Nayo ni mfano wa moyo. Imefananishwa na kioo kwa kuwa imekusanya sifa ambazo zimo katika moyo wa muumini, nazo ni usafi na unyenyekevu. Hivyo huona haki na uongofu kwa sababu ya usafi. Hupatikana ndani yake huruma, rehema na upole kwa sababu ya unyenyekevu wake. Hupigana vita na maadui wa Allaah (Ta´ala), huwa mshupavu kwao, huwa mkali juu ya haki na mwenye msimamo thabiti juu yake. Sifa moja haibatilishi nyingine wala hazipingani – bali husaidiana na kusapotiana:

أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ

”Wakali kwa makafiri wanahurumiana baina yao.”[1]

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelikukimbia.”[2]

Imekuja katika masimulizi:

“Mioyo ni vyombo vya Allaah (´Azza wa Jall) katika ardhi Yake. Basi yenye kupendwa zaidi Kwake ni laini zaidi, imara zaidi na safi zaidi.”[3]

Sambamba na moyo huu kuna mioyo miwili inayozingatiwa kuwa ya kusimangwa katika hali mbili zilizo kinyume:

1 – Moyo wa jiwe. Ni moyo mgumu usiyo na huruma, ihsani wala wema. Hauna usafi wa kuiona haki. Bali ni wenye kiburi na wenye ujinga. Hauijua haki na wala hauna huruma kwa viumbe.

2 – Moyo dhaifu na wenye maji. Hauna nguvu wala msimamo. Bali hukubali kila sura. Hauna nguvu ya kuhifadhi sura hizo wala nguvu ya kuathiri wengine. Huathirika na kila kinachochanganyika nacho, kiwe chenye nguvu au dhaifu, kilicho kizuri au kibaya.

[1] 48:29

[2] 03:159

[3] at-Twabaraaniy katika “Musnad-ush-Shaamiyyiyn” (2/19). Cheni ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa al-´Iraaqiy katika “al-Mughniy ´an Haml-il-Aswfaar” (2/1691), cheni yake ya wapokezi ni yenye nguvu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (1691).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 120-122
  • Imechapishwa: 24/08/2025