Inapokuwa siku ya Tarwiyah[1], ambaye ametoka katika Ihraam huingia tena katika Ihraam kutoka Makkah na hutoka kwenda ´Arafah. Jua linapopinduka siku ya ´Arafah, huswali Dhuhr na ´Aswr kwa kuzijumuisha pamoja kwa adhaana moja na Iqaamah mbili. Kisha huenda katika mahali pa kusimama. ´Arafah yote ni mahali pa kusimama isipokuwa sehemu ya chini ya ´Uranah.

Inapendekezwa kusimama katika mahali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposimama au karibu na hapo juu ya mlima, karibu na mawe na aweke njia ya watembea kwa miguu mbele yake. Aelekee Qiblah na awe amepanda kipando. Azidishe kusema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير

“Hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika. Ufalme ni Wake, sifa zote njema ni Zake na Yeye ni Muweza wa kila kitu.”[2]

Ajitahidi katika kuomba na kujinyenyekeza kwa Allaah (´Azza wa Jall) mpaka jua lizame. Kisha aondoke pamoja na kiongozi kwenda Muzdalifah kupitia njia yenye msongamano, akiwa na utulivu na heshima. Aendelee kuleta Talbiyah na kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).

[1] Tarehe 8 Dhul-Hijjah.

[2] at-Tirmidhiy (3585) na Ahmad (2/210). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3585).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 09/11/2026