Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:
104 – Kila kitu kinatokea kwa matakwa ya Allaah (Ta´ala), ujuzi, mipango na makadirio Yake.
105 – Matakwa Yake yameshinda matakwa yote. Mipango Yake imeshinda nguvu zote. Anafanya akitakacho na si mwenye kudhulumu.
106 – Anatakasa kutokamana na kila ovu na kilichoharibika, kila chenye kasoro na mapungufu:
لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ
“Haulizwi kwa yale Anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[1]
MAELEZO
Ibn Abiyl-´Izz amesema:
”Yale yanayofahamishwa na Qur-aan ambapo Allaah anajitakasa kutokana na kuwadhulumu waja, kunapelekea maoni ya kati na kati baina ya maoni ya Qadariyyah na ya Jabriyyah. Zile dhuluma na mambo mabaya wanayofanyiana wanadamu sio dhuluma na mabaya kutokana Naye, kama wanavodhania Qadariyyah, Mu´tazilah na wengineo. Kwani mtazamo huo ni kumlinganisha Allaah na viumbe Wake. Yeye ni Mola mkwasi na muweza ilihali wao ni waja mafukara na wenye kudhalilishwa.
Wala dhuluma sio kitu kisichowezekana ambacho hakijumuishwi na uwezo, kama wanavosema wanafalsafa na wengineo. Wanaona kuwa haiwezekani dhuluma ikawepo katika yale mambo yenye kuwezekana na yaliyokwishakadiriwa. Bali kila chenye kuwezekana – endapo Angelifanya hivo – basi Kwake ni uadilifu. Kwani dhuluma haiwi isipokuwa kutoka kwa ambaye imeamrishwa na kukatazwa na mwengine, na hilo haliwi kwa Allaah. Maoni hayo yanaraddiwa na maneno Yake (Ta´ala):
وَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا يَخَافُ ظُلْمًا وَلَا هَضْمًا
”Na yeyote atakayetenda mema naye ilihali ni muumini, basi hatokhofu dhuluma wala kupunjwa.”[2]
مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ
”Haibadilishwi kauli Kwangu, Nami si Mwenye kudhulumu katu waja.”[3]
وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا هُمُ الظَّالِمِينَ
”Na wala hatukuwadhulumu, lakini walikuwa wao wenyewe ndio madhalimu.”[4]
وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا
“… na Mola wako hamdhulumu yeyote.”[5]
الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۚ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ
“Hii leo kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyachuma – hakuna dhuluma leo hii! Hakika Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu.”[6]
Vilevile yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:
”Enyi waja Wangu! Hakika Mimi nimejiharamishia dhuluma juu ya nafsi Yangu na kuifanya kati yenu kuwa ni haramu. Hivyo basi, msidhulumiane.”[7]
Hapa kumefahamishwa mambo mawili:
1 – Amejiharamishia dhuluma juu ya nafsi Yake, jambo ambalo halipatikani kwa kitu kisichowezekana.
2 – Ameleeza kuwa amejiharamishia juu ya nafsi Yake kama ambavo ameeleza kuwa amejifaradhishia juu ya nafsi Yake huruma. Haya yanaraddi nadharia yao inayosema kuwa dhuluma haiwi isipokuwa kutoka kwa ambaye imeamrishwa na kukatazwa na mwengine, na hilo haliwi kwa Allaah. Wanatakiwa kuambiwa kuwa Yeye (Subhaanah) amejifaradhishia juu ya nafsi Yake huruma kama jinsi amejiharamishia juu ya nafsi Yake dhuluma. Amejifaradhishia na kujiharamishia juu ya nafsi Yake yale ambayo Anayaweza, na si yale ambayo hayawezekani kabisa Kwake.”[8]
[1] 21:23
[2] 20:112
[3] 50:29
[4] 43:76
[5] 18:49
[6] 40:17
[7] Muslim (2577) na Ahmad (5/160).
[8] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 659-670
- Muhusika: Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – al-Albaaniy
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 97-99
- Imechapishwa: 16/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)