64. Nuru ya ulimwengu siku ya Qiyaamah

Amesema (Ta´ala):

وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا

”Ardhi itang’ara kwa nuru ya Mola wake.”[1]

Basi atakapokuja (Tabaarak wa Ta´ala) siku ya Qiyaamah ili ahukumu baina ya waja Wake, ardhi itang’aa kwa nuru Yake. Nuru hiyo si ya jua wala ya mwezi, kwani jua litafungwa na mwezi utaingia kasoro na nuru yao itaondoka. Pazia Lake (Subhaanahu wa Ta´ala) ni nuru. Abu Muusa (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Allaah halali na wala haimstahikii Yeye kulala. Anaishusha mizani na kuinyanyua. Kwake kunapandishwa matendo ya usiku kabla ya mchana na matendo ya mchana kabla ya usiku. Pazia Yake ni Nuru; lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila anachoona katika uumbaji Wake.” Kisha akasoma:

أَن بُورِكَ مَن فِي النَّارِ وَمَنْ حَوْلَهَا وَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Amebarikiwa aliye karibu na moto na aliye pembezoni mwake – na utakasifu ni wa Allaah, Mola wa walimwengu!”[2]

Kwa hiyo kung’aa kwa pazia hilo ni kwa sababu ya nuru ya uso Wake; lau kama si kwa ajili yake, basi miale ya uso Wake na nuru Yake ingeziteketeza kila kitu macho Yake yanayofikia. Kwa ajili hiyo wakati Yeye (Tabaarak wa Ta´ala) alipojionyesha kwa mlima na akaondosha sehemu kidogo tu ya pazia, basi mlima ulizama ardhini na ukasambaratika – haukuweza kusimama mbele Yake (Tabaarak wa Ta´ala). Hii ndio maana ya maneno yake Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhum) kuhusu tafsiri ya maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارَ

“Macho hayamzunguki.”[3]

Akasema:

”Huyo ni Allaah (´Azza wa Jall); Anapojidhihirisha kwa nuru Yake basi hakuna kitu kinachoweza kusimama mbele Yake.”[4]

Hilo ni kutokana na umakini na ufahamu wa ajabu wa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Vipi isiwe hivyo hali ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwombea du´aa Allaah amfunze tafsiri!

Kwa hiyo Mola (Tabaarak wa Ta´ala) ataonekana kwa macho siku ya Qiyaamah, hata hivyo haitowezekan macho yakamzunguka Yeye. Uzungukaji ni kitu cha ziada ya uoni. Allaah ana wasifu wa juu zaidi tupigie mfano wa jua ambalo tunaliona lakini hata hivyo hatulizunguki kama lilivyo wala hata karibu na kuzunguka uhalisia wake. Kwa ajili hiyo wakati bwana mmoja alipomuuliza Ibn ´Abbaas kuhusu Kuonekana na akamjengea hoja kwa:

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارَ

“Macho hayamzunguki.”,

alimuuliza: ”Je, wewe unaiona mbingu? Akasema: ”Ndio.” Akamuuliza: ”Unalizunguka?” Akasema: ”Hapana.” Ndipo akasema: ”Allaah (Ta´ala) ni mkubwa na mtukufu zaidi!”

[1] 39:69

[2] 27:8 Muslim (179).

[3] 6:103

[4] at-Tirmidhiy (3279).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 116-119u
  • Imechapishwa: 24/08/2025