64. Fadhilah za ukubwa wa mkusanyiko na namna ya kupanga safu katika swalah ya jeneza

63- Kila ambavo mkusanyiko utakuwa mkubwa zaidi ndivo itakuwa bora na manufaa zaidi kwa maiti. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna maiti yeyote ambaye ataswaliwa na kundi la waislamu ambao wanafika mia ambapo wote wakamuombea isipokuwa watakubaliwa.”

Imekuja katika Hadiyth nyingine:

“… atasamehewa.”

Ameipokea Muslim (03/53), an-Nasaa´iy (01/281, 282), at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha (02/143, 144), al-Bayhaqiy (04/30), at-Twayaalisiy (1526), Ahmad (06/32, 40, 97, 231) kupitia kwa ´Aaishah kwa tamko la kwanza.

Ameitoa pia Muslim, an-Nasaa´iy, al-Bayhaqiy na Ahmad (03/266) kupitia kwa Anas. Pia Ibn Maajah (01/453) kupitia kwa Abu Hurayrah kwa tamko jengine. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

Maiti anaweza kusamehewa pia ikiwa ni idadi chini ya mia ikiwa ni waislamu ambao hawakuichanganya Tawhiyd yao na chochote katika shirki. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna mtu yeyote katika waislamu anayekufa wakasimama katika jeneza lake watu arubaini ambao hawamshirikishi Allaah na chochote isipokuwa Allaah atawakubalie maombezi yao kwa ajili yake.”

Ameipokea Muslim, Abu Daawuud (02/64), Ibn Maajah, al-Bayhaqiy na Ahmad (2509) kupitia kwa Ibn ´Abbaas.

Ameipokea pia an-Nasaa´iy na Ahmad (06/331, 334) kupita kwa Maymuumah, mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa mukhtasari. Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

64- Imependekezwa wapange safu tatu[1] na zaidi ya hapo nyuma ya imamu. Hilo ni kutokana na Hadiyth mbili zilizopokelewa juu ya hilo:

Ya kwanza: Abu Umaamah ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswalia jeneza wakiwa watu saba ambapo akafanya watatu safu, wawili safu na wawili wengine safu.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr”. al-Haythamiy amesema katika “al-Majma´” (03/432):

“Ndani yuko Ibn Lahiy´ah” na ametiwa midomoni.”

Hilo ni kwa upande wa hifdhi yake. Vinginevyo hatuhumiwi kwa nafsi yake. Kwa hiyo Hadiyth zake katika shawahidi hazina ubaya. Kwa ajili hiyo nimeitaja hali ya kuitolea ushahidi Hadiyth inayofuata ambayo ni:

Ya pili: Maalik bin Hubayrah amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote anayekufa akaswaliwa na safu tatu za waislamu isipokuwa itawajibika.” [Katika upokezi mwingine imekuja: “Atasamehewa.”

Akasema: (Marthad bin ´Abdillaah al-Yazaniy):

“Maalik pindi watu wa jeneza wanapokuwa wachache basi anawapanga safu tatu.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/63) na mtiririko ni wake, at-Tirmidiy (02/143), Ibn Maajah (01/454), Ibn Sa´d (07/420), at-Twabaraaniy (19/258-665), Abu Ya´alaa (6731), al-Haakim (01/362, 363), al-Bayhaqiy (04/30), Ahmad (04/79), tamko la mwisho ni lake na vivyo hivyo katika upokezi wa al-Bayhaqiy na al-Haakim ambaye amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye. at-Tirmidhiy amesema akifuatwa na an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/212):

“Hadiyth ni nzuri.”

al-Haafidhw akamkubalia katika “al-Fath” (03/145). Ndani yake wote hao yumo bwana mmoja kwa jina Muhammad bin Ishaaq. Hadiyth zake ni nzuri muda wa kuwa atasimulia Hadiyth kwa kuweka wazi. Lakini hapa ametaja kwa kutokuweka wazi. Sijui ni kivipi wameifanya Hadiyth hiyo kuwa ni nzuri, sembuse kuisahihisha?

65- Imamu asipokuwa na mtu mwengine zaidi ya mwanamme mmoja tu, basi asisimame sambamba naye kama ilivyo Sunnah katika swalah nyenginezo. Bali atasimama nyuma ya imamu. Hilo ni kutokana na Hadiyth iliotangulia katika masuala ya 62 na humo imekuja:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatangulia mbele, Abu Twalhah alikuwa nyuma yake, Umm Sulaym alikuwa nyuma ya Abu Twalhah na hapakuwa mwengine zaidi yao.”

[1] ash-Shawkaaniy (04-47) amesema:

”Uchache wa kinachoitwa safu ni wanamme wawili. Hakuna mpaka wa wingi wake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 127-128
  • Imechapishwa: 17/08/2020