Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Atakuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Qiyaamah na nyombezi tatu:

1 – Atawaombea wale watu waliosimama katika kiwanja cha Mkusanyiko. Watu watamwendea Aadam, Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysa bin Maryam (´alayhimus-Salaam) na kuwaomba wawaombee, lakini wataomba udhuru mpaka iishilie kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atakuwa na nyombezi tatu:

1 – Uombezi mkubwa juu ya wale watu wataokuwa katika uwanja wa Mkusanyiko ili kuhukumiwe na kufanyiwa hesabu baina yao. Haya yatakuwa baada ya Mtume Aadam, Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysaa bin Maryam kuomba udhuru. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ndiye bwana wa watu siku ya Qiyaamah? Mnajua ni kwa nini? Siku ya Qiyaamah Allaah atawakusanya watu wote sehemu moja. Watamsikia mwitaji, macho yao yamekodolewa na jua litasogezwa karibu nao. Baadhi ya watu watasema: ”Hivi hamuoni yale mliyomo? Hivi hamtazami ni nani awezaye kuwaombea mbele ya Mola wenu?” Baadhi ya watu watasema: ”Baba yenu Aadam.” Waende kwa Aadam na waseme: “Ee Aadam! Hakika wewe ndiye baba wa watu. Allaah amekuumba kwa mkono Wake, akakupulizia roho Yake na akawaamrisha Malaika kukusujudia. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Aadam atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Alinikataza kula katika mti ambapo nikamuasi. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Nuuh.” Waende kwa Nuuh na kusema: “Ee Nuuh! Wewe ndiye Mtume wa kwanza kutumilizwa ardhini. Allaah amesema kuwa wewe ni mja mwenye kushukuru. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Nuuh atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Nilikuwa na haki ya du´aa yenye kuitikiwa na nikaiomba dhidi ya watu wangu. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Ibraahiym.” Waende kwa Ibraahiym na kusema: “Ee Ibraahiym! Wewe ni kipenzi mwandani kabisa wa Allaah na Mtume Wake ardhini. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Ibraahiym atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake.” Atataja kusema kwake uongo mara tatu kisha atasema: “Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muusa.” Waende kwa Muusa na kusema: “Ee Muusa! Wewe ni Mtume wa Allaah! Allaah amekuteua kutokamana na watu wengine wote kwa ujumbe na maneno Yake. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Muusa atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Niliua nafsi bila idhini. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa ´Iysaa.” Waende kwa ´Iysaa na kusema: “Ee ´Iysaa! Wewe ni Mtume wa Allaah. Uliwazungumzisha watu katika hali ya uchanga. Wewe ni neno Lake alilolirusha kwa Maryam na roho inayotokamana Naye. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” ´Iysaa atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muhammad.” Waende kwa Muhammad na kusema: “Ee Muhammad! Wewe ni Mtume wa Allaah na Nabii wa mwisho. Allaah amekusamehe dhambi zako zote. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Nitaondoka mpaka nitakapofika chini ya ´Arshi ambapo nitasujudu mbele ya Mola wangu. Kisha Allaah ataniidhinisha kumhimidi kwa njia ambayo hajapatapo kuhimidiwa na mwingine yeyote. Ataambiwa: “Ee Muhammad! Inua kichwa chako. Uliza utapewa, omba utapokelewa uombezi wako.” Nitainua kichwa changu na kusema: “Ee Allaah! Ummah wangu! Ummah wangu!” Kutasemwa: “Ee Muhammad! Wale ambao katika Ummah wako ambao hawatofanyiwa hesabu waingize Peponi kupitia milango yake ya kulia. Milango mingine yote ya Peponi watashirikiana na wengineo.” Naapa kwa Yule ambaye mkononi Mwake iko roho yangu umbali kati ya milango miwili ya Pepo ni kama umbali kati ya Makkah na Hajar, au ni kama umbali kati ya makkah na Busraa.”[1]

[1] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (194).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 95-97
  • Imechapishwa: 02/11/2024