Mwenye kutaka kuingia ndani ya Ihraam, inapendekezwa kwake kuoga, kujisafisha, kujipaka manukato, kuvua nguo iliyoshonwa kwa ajili ya mwili na kuvaa shuka ya chini na shuka ya juu nyeupe na safi. Kisha ataswali Rak´ah mbili na ataingia ndani ya Ihraam baada yake. Kuingia katika Ihraam ni kuazimia kuingia katika ´ibaadah hiyo. Inapendekezwa kutamka ´ibaadah aliyoingia nayo katika Ihraam na kuweka sharti, akisema:

“Ee Allaah! Hakika mimi ninataka kufanya ´ibaadah hii. Ikiwa kizuizi kitanizuia, basi mahali pa kutoka katika Ihraam kwangu ni pale utakaponizuia.”

Ana uchaguzi kati ya Tamattu´, Ifraad na Qiraan. Bora zaidi ni Tamattu´, kisha Ifraad, kisha Qiraan.

Tamattu´ ni kuingia ndani ya Ihraam kwa ajili ya ´Umrah katika miezi ya Hajj, kuimaliza ´Umrah, kisha kuingia ndani ya Ihraam kwa ajili ya Hajj katika mwaka huo. Ifraad ni kuingia ndani ya Ihraam kwa ajili ya Hajj peke yake. Qiraan ni kuingia ndani ya Ihraam kwa ajili ya Hajj na ´Umrah pamoja au kuingia katika Ihraam kwa ajili ya ´Umrah kisha kuingiza Hajj ndani yake. Ikiwa ataingia katika Ihraam kwa ajili ya Hajj kisha akaingiza ´Umrah ndani yake, Ihraam yake ya ´Umrah haitasihi. Anapokaa sawasawa juu ya kipando chake, atasema Talbiyah:

لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد، والنعمة، لك والملك، لا شريك لك

“Ee Allaah! Nimeitikia wito Wako, nimeitikia wito Wako. Nimeitikia wito Wako, huna mshirika, nimeitikia wito Wako. Hakika himdi zote njema ni Zako, neema ni Yako na ufalme ni Wako. Huna mshirika.”

Inapendekezwa kuleta Talbiyah kwa wingi na wanaume kuinua kwayo sauti, si kwa wanawake. Inasisitizwa zaidi anapopanda sehemu ya juu, anaposhuka bondeni, anaposikia mtu akisema Talbiyah, anapofanya jambo lililokatazwa katika Ihraam kwa kusahau au anapokutana na msafara na baada ya swalah za faradhi, wakati wa mwisho wa usiku na mwanzo wa usiku na mchana.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 45
  • Imechapishwa: 05/11/2026