Swali: Ni ipi hukumu ya mtu anayewachukia watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawapendi?

Jibu: Hili ni maovu makubwa na halijuzu. Inalazimika kumpenda mtu kwa ajili ya Allaah na kumchukia kwa ajili ya Allaah. Hili si maalum kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pekee, bali ni juu ya kila muislamu: awapende waumini na awachukie makafiri na awapende watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walio waumini. Ama yule ambaye ni kafiri miongoni mwao, basi huyo anachukiwa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mfano Abu Lahab ni katika familia yake, lakini anachukiwa kwa ajili ya Allaah. Mfano mwingine Abu Twaalib pia ni katika watu wa familia yake, lakini anachukiwa kwa ajili ya Allaah. Wanapendwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walio waumini kama ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), al-Hasan, al-Husayn, Faatwimah na wengineo waliokuja baada yao katika waumini mpaka leo hii miongoni mwa kizazi cha Haashim. Wanapendwa kwa ajili ya Allaah kama wanavyopendwa waumini wengine, bila kujali nasaba zao. Yule ambaye ni kafiri anachukiwa kwa ajili ya Allaah, hata kama ni miongoni mwa watoto wa Manabii. Hivyo upendo na chuki vinategemea utiifu kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), si kwa nasaba. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakukumbusheni juu ya Allaah juu ya watu wa familia yangu.”

Kwa maana kuwapenda, kuwapa haki zao na kutowaudhi.

Kadhalika waumini wote wanapaswa kupendwa kwa ajili ya Allaah na wasidhuriwe. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا

“Wale wanaowaudhi waumini wa kiume na waumini wa kike pasi na wao kufanya kosa lolote, basi kwa hakika wamejibebea uzushi mkuu wa dhuluma na dhambi ya wazi.”[1]

Lakini Raafidhwah na watu wanaofanana nao wanaona kwamba asiyepitiliza katika kuwatukuza  au asiyewaabudu watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi huyo anawachukia. Hili ni katika ujinga na upotofu wao. Watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawaabudiwi badala ya Allaah, si ´Aliy wala mwingine yeyote anayestahiki kuabudiwa. ´Ibaadah ni haki ya Allaah pekee, hana mshirika. Hata Manabii hawabudiwi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamrisha ya kwamba, msiabudu yeyote isipokuwa Yeye pekee.”[2]

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.”[3]

فَادْعُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Basi mwombeni Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”[4]

Jengine ni kwa mujibu wa Raafidhwah na mfano wao katika Baatwiniyyah wanaona kuwa yule asiyeona kuwa maimamu kumi na wawili wanajua mambo yaliyofichikana na kwamba wamekingwa na makosa eti anawachukia, jambo ambalo ni ujinga na upotofu. Hawajui ghaibu na wala hawakukingwa na kukosea. Kujua ghaibu ni kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee. Yeyote anayesema kuwa ´Aliy, al-Hasan, al-Husayn au wengine wanajua ghaibu, huyo ni kafiri ambaye amekosea vibaya na amepotea. Haijalishi kitu ni Raafidhwah au mwengine yeyote. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ

“Sema: “Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye yaliyofichikana isipokuwa Allaah.”[5]

[1] 33:58

[2] 17:23

[3] 01:05

[4] 39:02

[5] 27:65

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3333/حكم-بغض-ال-البيت-وعداوتهم
  • Imechapishwa: 05/11/2026