Kwa haya muumini anapata kujua kuwa ni wajibu kwake kupupia juu ya kutafuta sababu za kusalimika na kwamba hili ni khatari kubwa, ni mamoja yanayohusu Hodhi na Njia. Ni wajibu kwake kumuomba Allaah mwisho mwema. Vilevile ajitahidi kuwa na uimara katika haki na awe na msimamo juu yake. Sambamba na hilo atahadhari na kumuasi Allaah (´Azza wa Jall) na akimbilie kutubia. Kila pale anapoteleza kutenda dhambi basi akimbilie kutubia. Hakuna yeyote aliyekingwa na kukosea. Lakini pamoja na hivyo ni lazima kuleta tawbah. Kila atapofanya mapungufu au dhambi aharakishe kufanya tawbah:
وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ
“Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao, basi humdhukuru Allaah wakaomba msamaha kwa madhambi yao – na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah? – na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua. Hao malipo yao ni msamaha kutoka kwa Mola wao na Pepo zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo – uzuri ulioje ujira wa watendaji wema!” (03:135-136)
Muumini anatakiwa kuihesabu nafsi yake siku zote, aichunge na kuipeleleza. Asijikweze na kumfanya akajiaminisha. Badala yake anatakiwa kuihesabu nafsi yake na kupambana nayo. Huenda kwa kufanya hayo akasalimika.
وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ
“Na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika kwa Mola wao ni wenye kurejea – Hao wanakimbilia katika kufanya kheri nyingi nao wao katika hayo watawatangulia [wengine].” (23:60-61)
Ibn Abiy Mulaykah amesema:
“Nilikutana na Maswahabah thelathini wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao wote walikuwa wanachelea unafiki juu ya nafsi zao. Hakukuwa miongoni mwao ambaye alikuwa anasema kwamba ana imani kama ya Jibriyl na Mikaaiyl.”[1]
Ibraahiym at-Taymiy amesema:
“Sijapatapo kuyalinganisha maneno yangu na matendo yangu isipokuwa nilichelea nisije kuwa mwongo.”[2]
Kwa hivyo ni wajibu ni kuhadhari na mtu asijiamini na kujikweza kutokana na matendo yake. Hakika si vyenginevyo Allaah anakubali tu kutoka kwa wachaji Allaah. Mtu apambane na nafsi yake. Atambue mapungufu na kasoro zake ili aweze kujitahidi, aijue haki na alazimiane na tawbah mpaka pale atapokutana na Mola Wake hali ya kuwa radhi naye.
[1] al-Bukhaariy (47).
[1] al-Bukhaariy (47).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 92-93
- Imechapishwa: 02/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)