Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Njia imewekwa juu ya Jahannam na ni daraja iliyo baina ya Pepo na Moto. Watu watapita juu yake kadiri ya matendo yao. Kuna ambao watapita kama kufumba na kufumbua, wengine kama umeme, wengine kama upepo, wengine kama mpanda farasi, wengine kama mwenye kusafiri kwa ngamia, wengine kama mkimbiaji, wengine kama watembeaji, wengine kama mtambaaji na wengine watashikwa na kutupwa Motoni. Daraja inayo ndoano zinazowanyakua watu kwa mujibu wa matendo yao. Yule atakayevuka Njia ataingia Peponi.
Watapoivuka daraja hiyo watasimama juu ya daraja, baina ya Pepo na Moto, na kulipizana kisasi wao kwa wao. Baada ya kusafishwa, ndio watapewa idhini ya kuingia Peponi.
MAELEZO
Njia itawekwa juu ya Moto wa Jahannam. Atayeanguka kwenye Njia hii anatumbukia Motoni. Njia hii itapitiwa juu yake na kila mwenye kuingia Peponi. Amesema (Ta´ala):
وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا
“Na hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa ataufikia. Hiyo kwa Mola wako ni hukumu ya lazima kutimizwa. Kisha Tutawaokoa wale wenye kumcha Allaah na tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti.” (19:71-72)
Waumini watapita na kuokoka. Wasiokuwa waumini hawatopita. Kinyume chake wataanguka Motoni. Wale wataopita juu ya Njia hii kuna waumini ambao watapita kama kufumba na kufumbua. Wengine watapita kama umeme, wengine kama mpanda farasi, wengine kama upepo na wengine kama ngamia. Kila mmoja atapita juu yake kutegemea na vile matendo yake yalivyo. Vilevile kuna wengine watapita kwa kujikongoja; mara amesimama na wakati mwingine anajikwaa. Kuna wengine watapita na kutumbukizwa Motoni. Kila mmoja atapita kutegemea na matendo aliokuwa juu yake. Waumini wakweli tu ndio wataokoka. Waliosalia watatupwa Motoni. Kuna ambao utawaonja kidogo lakini hatimaye watasalimika. Kuna wengine watatumbukia humo na kuadhibiwa kwa kiwango cha madhambi yao na halafu baadaye Allaah awatoe Motoni na kuwaingiza Motoni. Hakuna atayedumishwa Motoni milele isipokuwa makafiri peke yao.
Kuhusiana na waislamu watenda madhambi wataotumbukia humo wataadhibiwa kwa muda fulani kila mmoja kwa kiasi cha madhambi yake. Kisha Allaah atawapa idhini waombezi wawaombee. Miongoni mwa watu hao ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye atawaombea halafu watolewe Motoni. Ataombea nyombezi nne. Kila uombezi Allaah atampa idadi ya watu maalum ambao watatolewa Motoni. Baada ya hapo Motoni kutabaki watu katika ummah huu ambao hawakupata uombezi wowote. Pamoja na hivyo Allaah atawatoa humo kutokana na fadhila na huruma Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Atawatoa Motoni na kuwaingiza Peponi. Watawekwa kwenye mto wa uhai. Mto huo unaitwa “mto wa Uhai”. Wakiwekwa humo watachipuka kama inavyochipuka mbegu kwenye tope la mafuriko. Umbile lao likitimia ndipo wataidhinishwa sasa kuingia Peponi[1].
[1] al-Bukhaariy (6560) na Muslim (184).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 90-92
- Imechapishwa: 28/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)