Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nguzo zake ni sita: Kumuamini Allaah…

MAELEZO

Kumuamini Allaah kumekusanya mambo manne:

1- Kuamini uwepo wa Allaah. Vipo vitu vinne vinavyojulisha juu ya uwepo wa Allaah:

  1. Maumbile.
  2. Akili.
  3. Shari´ah.
  4. Hisia.

Kuhusiana na dalili za kimaumbile, zinathibitisha uwepo Wake kwa njia ifuatayo:

Kila kiumbe ameumbwa kwa umbile la kumuamini Mola Wake, pasi na kutanguliwa na kufikiri au kujifunza. Hakuna mwingine isipokuwa tu yule mwenye kupata kitu katika upotevu moyoni mwake ndio huenda kinyume na maumbile haya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mtoto yoyote isipokuwa huzaliwa juu ya maumbile. Baadaye ni wazazi wake ndio humfanya kuwa myahudi, mnaswara au mwabudu moto.”[1]

Ama kuhusiana na dalili ya kiakili inayothibitisha uwepo wa Allaah, ni jambo lenye kutambulika kwamba viumbe vyote vilivyotangulia na kuja nyuma ni lazima viwe na Muumbaji. Haiwezekani kitu kikajileta chenyewe. Wala haiwezekani pia ikawa vimejileta patupu.

Ni jambo lisilowezekana kitu kikajileta chenyewe, kwa sababu hakuna kitu kinachoweza kujiumba chenyewe. Kwa sababu kabla ya kupatikana kwake hakikuwepo. Ni vipi basi ambacho hakikuwepo kitaumba?

Vilevile hakuna kitu chochote kinachoweza kujileta patupu. Kila chenye kujitokeza ni lazima kiwe na ambaye amekifanya kutokea. Jengine ni kwamba uwepo wake katika nidhamu hii ya kushangaza, mpangilio huu wenye kuambatana na mafungamano ya kisawasawa, ni dalili inayofahamisha kwamba ni jambo lisilowezekana kikawa kimetokea patupu. Kwa sababu kitu kilichokuja ghafla patupu hakiwi hata kwa katika mpangilio katika ule msingi wa uwepo wake, tusemeje juu ya hali ya kubaki na kuendelea kwake.

Ikiwa viumbe hivi haviwezi kuwa vimejileta vyenyewe wala kupatikana patupu, basi inalazimisha kuwa ni lazima viwe na Muumbaji, Naye si mwingine isipokuwa ni Allaah, Mola wa walimwengu.

Allaah ametaja dalili hii ya kiakili na hoja za kimaumbile katika Suurah “at-Twuur” pale aliposema:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote? Au wao wenyewe ndio waumbaji?” (at-Twuur 52 : 35)

Bi maana hawakuumbwa pasi na Muumba na wala sio wao wenyewe waliojiumba. Hivyo basi hili linawajibisha ya kwamba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ndiye Muumbaji wao. Kwa ajili hii Jubayr bin Mutw´im (Radhiya Allaahu ´anh) alisema pindi alipomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma Suurah “at-Twuur” na akafika katika Aayah hii:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَبِّكَ أَمْ هُمُ الْمُصَيْطِرُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote? Au wao wenyewe ndio waumbaji? Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini. Au wanazo hazina za Mola wako? Au wao ndio wenye mamlaka nayo?” (at-Twuur 52 : 35-37)

“Moyo wangu ulikuwa unakaribia kuruka na hapo ndio ilikuwa mara ya kwanza imani kuingia kwenye moyo wangu.”[2]

Wakati huo Jubayr alikuwa bado ni mshirikina.

Ameipokea al-Bukhaariy.

Hebu wacha tulete mfano utaoliweka hilo wazi zaidi. Lau mtu atakueleza kuhusu palasi ndefu lililojengwa na limezungukwa na mabustani na ambalo mito inapita kati yake. Limejazwa magodoro na vitanda na limepambwa kwa kila aina ya mapambo. Baada ya hapo mtu huyu akakwambia ya kwamba palasi hii na yote yaliyo ndani yake vimejileta vyenyewe au vimetoka patupu, basi papo hapo ungelikanusha hilo, kumkadhibisha na ungezingatia maneno yake hayana maana yoyote. Je, inawezekanaje  kwa ulimwengu huu mpana kwa ardhi zake, mbingu zake, nyota zake na mpangilio wake na  hali zake zenye kusifika iwe kwamba umejileta wenyewe au patupu na pasi na Muumbaji?

Ama kuhusiana na dalili za Kishari´ah zenye kuthibitisha uwepo wa Allaah, yapo katika Vitabu vyote vilivyoteremshwa. Vyote hivo na hukumu ilizonavyo zilizo na manufaa kwa viumbe ni dalili inayoonyesha kuwa zinatoka kwa Mola wa hekima ambaye ni mjuzi wa manufaa ya viumbe Wake. Isitoshe maelezo yake ya kilimwengu ambayo hali ya leo imeshuhudia juu ya usahihi na ukweli wake, ni dalili tosha zinazoonyesha kuwa ni zenye kutoka kwa Mola ambaye ni Muweza wa kuumba yale aliyoyatolea maelezo.

Ama dalili za kihisia zenye kuthibitisha uwepo wa Allaah, ni kwa njia mbili:

1- Sisi tunasikia na tunajionea wenyewe namna ambavyo du´aa za wenye kuomba zinaitikiwa na namna ambavo shida za wenye matatizo wanavyosaidiwa. Hii ni dalili ya wazi inayofahamisha juu ya uwepo wa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَنُوحًا إِذْ نَادَىٰ مِن قَبْلُ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ

“Na kumbuka Nuuh! Pindi alipoita kabla ambapo Tukamuitikia.” (al-Anbiyaa´ 21 : 76)

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ

“Na pindi mlipomuomba uokozi Mola wenu Naye akakujibuni.”  (al-Anfaal 08 : 09)

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Kuna bedui mmoja aliingia siku ya ijumaa na huku Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko anatoa Khutbah na akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mali zimeangamia na familia zimekuwa na njaa. Tuombee kwa Allaah.” Akanyanyua mikono yake na akaomba. Ghafla mawingu yajikusanya kama mfano wa jibali. Hakuwahi kuteremka kutoka juu ya minbari yake kabla ya mvua kuteremka kwenye ndevu zake. Katika ijumaa ya pili akaja bedui yuleyule, au mwingine, na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Nyumba zimebomoka na mali imeangamia. Tuombee kwa Allaah.” Akanyanyua mikono yake na kuomba: “Ee Allaah! Pembezoni mwetu na si juu yetu!” Hakuashiria katika upande wowote, isipokuwa ilisimama.”[3]

Mpaka hii leo kujibiwa du´aa za wenye kuomba ni jambo linaloshuhudiwa kwa yule mwenye kurejea kwa Allaah (Ta´ala) kikweli na akatimiza sharti za kujibiwa.

2- Alama za Mitume, ambazo pia huitwa “miujiza”, ambazo watu wameziona na kuzisikia, ni dalili za wazi kabisa juu ya uwepo wa Yule aliyewatuma. Naye si mwengine ni Allaah (Ta´ala). Mambo haya ni yenye kutoka nje ya uwezo wa mwanadamu. Allaah (Ta´ala) anayapitisha ili kuwatia nguvu na kuwanusuru Mitume Yake.

Mfano wa hilo ni miujiza ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah alimuamrisha kupiga fimbo yake kwenye bahari. Wakati alipofanya hivo, bahari ikagawanyika njia kumi na mbili na maji kati yake yakawa kama mfano wa kuta. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ ۖ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ

“Tukamteremshia Wahy Muusa kwamba: “Piga kwa bakora yako hiyo bahari!” – basi ikatengana ikawa kila sehemu kama jabali kubwa mno.” (ash-Shu´araa 26 : 63)

Mfano wa pili ni miujiza ya ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa akiwahuisha wafu na akiwatoa ndani ya makaburi yao kwa idhini ya Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Na nahuisha wafu kwa idhini ya Allaah.” (Aal ´Imraan 03 : 49)

وَإِذْ تُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِي

”… na ulipowatoa wafu kwa idhini Yangu.” (al-Maaidah 05 : 110)

Mfano wa tatu ni miujiza ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati Quraysh walipomtaka aonyeshe alama, akaashiria mwezi na ukagawanyika pande viwili. Watu wakauona. Amesema (Ta´ala) juu ya hilo:

اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ

”Saa imekaribia na mwezi umekatika! Na wanapoona alama hukengeuka na husema: “Uchawi unaoendelea” (al-Qamar 54 : 01-02)

Alama hizi za kihisia ambazo Allaah (Ta´ala) huzipitisha ili kuwatia nguvu na kuwanusuru Mitume Yake ni dalili ya wazi juu ya uwepo Wake (Ta´ala).

2- Kuamini uola Wake. Hii ina maana kuamini ya kwamba Yeye pekee ndiye Mola asiyekuwa na mshirika wala msaidizi.

Mola ni Yule mwenye kuendesha viumbe, ufalme na amri. Hakuna Muumbaji mwingine asiyekuwa Allaah. Hakuna mfalme mwingine isipokuwa Yeye. Hakuna mwamrishaji isipokuwa Allaah. Allaah (Ta´ala) Amesema:

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

“Zindukeni! Ni Vyake pekee uumbaji na amri.” (al-A´raaf 07 : 54)

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ

“Huyo basi Ndiye Allaah Mola wenu, ufalme ni Wake pekee.  Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende.” (Faatwir 35 : 13)

Haijulikani kwamba kuna kiumbe yeyote aliyekanusha uola wa Allaah (Subhaanah). Isipokuwa mtu mkaidi tu asiyeamini akisemacho. Kama ilivompitikia Fir´awn. Aliwaambia watu wake:

أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ

“Mimi ni mola wenu mkuu.” (an-Naazi´aat 79 : 24)

يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي

“Enyi wakuu! Sijui kama mnaye mungu badala yangu.” (al-Qaswasw 28 : 38)

Lakini pamoja na hivyo hakuwa ni mwenye kuyaamini moyoni. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا

“Wakazikanusha na hali ya kuwa nafsi zao zimeziyakinisha [yote hayo kwa sababu ya] dhuluma na majivuno.” (an-Naml 27 : 14)

Allaah ameeleza kuwa Muusa alisema kumwambia Fir´awn:

لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ بَصَائِرَ وَإِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا فِرْعَوْنُ مَثْبُورًا

“Kwa hakika umekwishajua kwamba hakuna Aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi kuwa ni dalili za kuonekana dhahiri. Na hakika mimi nakuona, ee Fir’awn, kuwa [karibuni] ni mwenye kuangamizwa!” (al-Israa´ 17 : 102)

Kwa ajili hii washirikina walikuwa wakikubali uola wa Allaah (Ta´ala), pamoja na kuabudu wengine asiyekuwa Yeye. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ يَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُون

“Sema: “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo humo, mkiwa mnaelewa? Watasema: “Ni vya Allaah pekee” Sema: “Je, basi hamkumbuki?” Sema: “Nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arshi tukufu?” Watesema: “Ni ya Allaah pekee” Sema: “Je, basi kwa nini hamwogopi? Sema: “Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu Naye ndiye alindae na wala hakilindwi chochote dhidi Yake, ikiwa mnaelewa?” Watasema: “Ni Allaah pekee” Sema: “Basi vipi mnazugwa?” (al-Muuminuun 23 : 84-89)

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ خَلَقَهُنَّ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ

“Ukiwauliza:  “Ni nani yule aliyeumba mbingu na ardhi?” Bila shaka watasema: “Ameziumba Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mjuzi wa kila kitu.” (az-Zukhruf 43 : 09)

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ فَأَنَّى يُؤْفَكُونَ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.” Basi ni wapi wanakogeuziwa!” (az-Zukhruf 43 : 87)

Amri ya Mola (Subhaanah) imeyaenea mambo ya kilimwengu na ya Kishari´ah. Kama jinsi Yeye ndiye mwenye kuendesha ulimwengu na anahukumu ndani yake kwa lile analolitaka kwa mujibu wa hekima Yake, kadhalika Yeye ndiye mwenye kuhukumu kwa Shari´ah ya ´ibaadah na hukumu za maisha ya kijamii kwa mujibu ilivyopelekea hekima Yake. Yule mwenye kufanya mtunga Shari´ah mwingine katika ´ibaadah badala ya Allaah au hakimu mwingine katika mambo ya miamala badala ya Allaah, basi atakuwa amemshirikisha na hakuhakikisha imani.

3- Kuamini uungu wa Allaah. Hii ina maana ya kwamba Yeye pekee ndiye mungu wa haki asiyekuwa na mshirika. Maana ya “mungu” ni yule mwenye kuabudiwa kwa mapenzi na kuadhimishwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Mungu wenu ni Mungu mmoja pekee; hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.” (al-Baqarah 02 : 163)

شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لا إِلَهَ إِلا هُوَ وَالْمَلائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِماً بِالْقِسْطِ لا إِلَهَ إِلا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah Ameshuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye na Malaika, na wenye elimu [wote wameshuhudia kwamba Yeye] ni Mwenye kusimamisha [uumbaji Wake] kwa uadilifu – hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.” (Aal ´Imraan 03 : 18)

Kila kinachoabudiwa badala ya Allaah basi uungu wake ni batili. Allaah (Ta´ala) amesema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

”Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye Mwenye haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.” (al-Hajj 22 : 62)

Kule kuitwa kwao “waungu” haina maana wana haki ya kuabudiwa. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu al-Laat, al-´Uzzaa na Manaat:

إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ

“Hayo si chochote isipokuwa ni majina mmeyaita (hayo masanamu) nyinyi na baba zenu, wala Allaah Hakuyateremshia madaraka yoyote.” (an-Najm 53 : 23)

Ameeleza kuwa Huud amesema kuwaambia watu wake:

أَتُجَادِلُونَنِي فِي أَسْمَاءٍ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا نَزَّلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ

“Hayo si chochote isipokuwa ni majina mmeyaita nyinyi na baba zenu; wala Allaah hakuyateremshia madaraka yoyote.” (al-A´raaf 07 : 71)

Ameeleza kuwa Huud alisema kuwaambia watu wake:

أَتُجَادِلُونَنِي فِي أَسْمَاءٍ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا نَزَّلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ

“Je, mnabishana nami juu ya majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu pasi na Allaah kuyateremshia kwayo mamlaka yoyote?” (al-A´raaf 07 : 71)

Ameeleza kuwa Yuusuf alisema kuwaambia marafiki zake gerezani:

أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ

“Je, waungu wengi wanaofarikiana ni bora au Allaah Mmoja pekee, mshindi Mwenye kudhibiti kila kitu? Hamwabudu pasi Naye isipokuwa majina mmeyaita nyinyi na baba zenu; hakuyateremshia Allaah kwayo mamlaka yoyote.” (Yuusuf 12 : 39-40)

Kwa ajili hii Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walikuwa wakiwaambia watu wao:

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika nyinyi hamna mungu mwengine badala Yake!”? (al-A´raaf 07 : 59)

Lakini washirikina waliyakataa haya. Badala yake wakaabudu wengine badala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuwaomba nusura na msaada. Allaah (Ta´ala) amebatilisha shirki ya washirikina kwa dalili mbili za kiakili:

1- Hakuna yeyote katika miungu hii ambaye ana kitu katika sifa ya kiungu. Imeumbwa na haiumbi. Haiwezi kuwaletea manufaa wale wenye kuiabudu na haiwezi kuwazuilia madhara. Haimiliki juu yao uhai wala kifo. Haimiliki chochote katika mbingu na wala hawana ushirika wowote. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً لَّا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا وَلَا يَمْلِكُونَ مَوْتًا وَلَا حَيَاةً وَلَا نُشُورًا

“Wakachukua pasi Naye miungu ambayo haiumbi chochote na hali wao wanaumbwa; wala hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao kujizuilia dhara wala kujipatia manufaa wala hawamiliki mauti wala kutoa uhai wala kufufuliwa.” (al-Furqaan 25 : 03)

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَمَا لَهُمْ فِيهِمَا مِن شِرْكٍ وَمَا لَهُ مِنْهُم مِّن ظَهِيرٍ وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ

“Sema: “Ombeni wale mnaodai kuwa ni miungu badala ya Allaah, hawamiliki uzito wa atomu mbinguni wala ardhini, na wala hawana humo ushirika na wala hana msaidizi miongoni mwao.” Na wala hautofaa uombezi mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini.” (Sabaa´ 34 : 22-23)

أَيُشْرِكُونَ مَا لَا يَخْلُقُ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَسْتَطِيعُونَ لَهُمْ نَصْرًا وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ

“Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu na hali wao wameumbwa na wala hawawezi kuwanusuru na wala hawawezi kujinusuru nafsi zao?” (al-A´raaf 07 : 191-192)

Ikiwa hali ya miungu hiyo ni kama hii, basi ni upumbavu mkubwa na batili kubwa kuiabudu.

2- Washirikina hawa walikuwa wakikubali kwamba Allaah (Ta´ala) pekee ndiye Mola na Muumba ambaye mikononi Mwake ndio mna ufalme wa kila kitu na ndiye mwenye kulinda na hakuna yeyote anayeweza kumlinda. Hili linalazimisha kwa wao kumwabudu Yeye pekee kama jinsi walivokuwa wakionelea kuwa ni Mmoja katika uola. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua.” (al-Baqarah 02 : 21-22)

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ فَأَنَّى يُؤْفَكُونَ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.” Basi ni wapi wanakogeuziwa!” (az-Zukhruf 43 : 87)

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ ۖ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai na nani anayeendesha mambo yote?   Watasema: “Ni Allaah”. Basi sema: “Je, basi kwa nini hamumchi?” Basi Huyo ndiye Allaah, Mola wenu wa haki. Na kuna nini baada ya haki isipokuwa upotevu? Basi vipi mnageuzwa?” (Yuunus 10 : 31-32)

4- Kuamini majina na sifa Zake. Hii ina maana ya mtu kuthibitisha majina na sifa ambazo Allaah amejithibitishia Yeye Mwenyewe katika Kitabu Chake au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia inayolingana na Yeye. Hayo yafanyike pasi na kupotosha, kukanusha, kuziletea namna wala kuzifananisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” (al-A´raaf 07 : 180)

وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Naye ana sifa za juu mbinguni na ardhini. Naye ni Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye hekima.” (ar-Ruum 30 : 27)

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (ash-Shuuraa 42:11)

Kuna makundi mawili yamepotoka katika jambo hili:

1- Kundi la kwanza: Mu´attwilah. Wanakanusha ima majina na sifa zote au baadhi yake. Wanadai kwamba kule kuyathibitisha kunalazimisha kumfananisha Allaah (Ta´ala) na viumbe Wake. Madai haya sio ya kweli kwa njia nyingi:

1- Nadharia yao inapelekea katika malazimisho ya batili. Moja ya batili hii ni kugongana kwa maneno ya Allaah (Subhaanah). Allaah (Ta´ala) amejithibitishia Yeye Mwenyewe majina na sifa kama jinsi amekanusha kuwepo kwa chochote kinachofanana Naye. Lau kuthibitisha majina na sifa kungelikuwa kunapelekea kumfananisha Allaah na viumbe, basi kungelipelekea pia kuwepo mgongano katika maneno ya Allaah na baadhi yakakadhibisha mengine.

2- Vitu viwili kuafikiana katika majina na sifa hakulazimishi viwe vinafanana. Mfano wa hilo ni watu wawili. Wote wawili ni watu wanaosikia, wanaona na wanazungumza. Hata hivyo hilo halilazimishi kwamba wanafanana katika maana ya utu, usikizi, uoni na maneno. Mfano mwingine ni wanyama. Wana mikono, miguu na macho. Lakini pamoja na hivyo haina maana mikono yao, miguu yao na macho yao vinafanana. Ikiwa tofauti kati ya viumbe, ambao wana majina na sifa moja, iko wazi na bainifu, basi tofauti kati ya Muumba na viumbe iko wazi na bainifu zaidi.

2- Kundi la pili: Mushabbihah. Wamethibitisha majina na sifa pamoja na kumfananisha Allaah (Ta´ala) na viumbe Wake. Wanadai kuwa nadharia yao ndio inaenda sambamba na maandiko, kwa kuwa si vinginevyo Allaah (Ta´ala) amewazungumzisha waja kwa njia ile wanayoifahamu. Madai haya ni batili kwa njia nyingi:

1- Kumfananisha Allaah (Ta´ala) na viumbe Wake ni jambo la batili ambalo linakataliwa na akili na Shari´ah. Haiwezekani maandiko ya Qur-aan na Sunnah kupelekea katika kitu ambacho ni batili.

2- Ni kweli kwamba Allaah (Ta´ala) amewazungumzisha waja kwa njia ile wanayoifahamu, lakini hili linahusiana na msingi wa maana ya dhati na sifa Zake. Lakini inapokuja katika uhakika wake na namna yake ambayo inaashiria maana hiyo, ni katika elimu anayoijua Allaah (Ta´ala) pekee na hakuna mwengine yeyoye anayeijua elimu hiyo.

Allaah akijithibitishia juu ya nafsi Yake kwamba ni Mwenye kusikia, basi hakika usikizi huu unajulikana kutokana na msingi wa ile maana, nako ni “kufikia ile sauti”. Lakini hata hivyo uhakika na namna ya usikizi wa Allaah hautambuliki. Kwa sababu uhakika na namna ya usikizi ni kitu kinatofautiana kutoka kwa kiumbe mmoja kwenda kwa kiumbe mwingine, basi kunapatikana tofauti kubwa juu ya hilo kati ya Muumba na viumbe.

Kwa hiyo Allaah (Ta´ala) anapojielezea Mwenyewe kwamba amelingana juu ya ´Arshi, kimsingi ni kwamba maana ya kulingana inajulikana. Lakini hata hivyo kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi hakujulikani kuhusiana na namna. Namna ya kulingana kwa viumbe kunatofautiana kwa kiumbe huyu na yule. Kulingana juu ya kiti sio kama kulingana juu ya ngamia mwenye ugumu wa kuondoka. Kukibainika tofauti hii kati ya viumbe, basi tofauti ni kubwa zaidi kati ya Muumba na viumbe.

Kumuamini Allaah (Ta´ala) kutokana na yale tuliyoyataja kunampa muumini matunda yafuatayo:

1- Kumuabudu Allaah (Ta´ala) pekee kwa njia ya kwamba mtu haweki matumaini yake kwa mwingine asiyekuwa Allaah, kumuogopa mwingine asiyekuwa Allaah, kumuabudu mwingine asiyekuwa Allaah na mengineyo

2- Kukamilika kwa mapenzi ya kumpenda Allaah (Ta´ala) na kumuadhimisha kutokana na majina Yake mazuri na sifa Zake kuu.

3- Kumuabudu Allaah pekee kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.

[1] al-Bukhaariy (1358) na (1359), Muslim (2658) na Ahmad (2/315).

[2] al-Bukhaariy (4854).

[3] al-Bukhaariy (1016) na Muslim (897).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 80-90
  • Imechapishwa: 01/06/2020