Hesabu itafanywa na Mola Wako (Jalla wa ´Alaa), ambaye ni al-Hakiym na al-´Adl (Mwenye hekima na Mwadilifu), hadhulumu punje hata kidogo. Amesema (Subhaanah):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hadhulumu uzito wa atomu. Na ikiwa ni [tendo] jema huizidisha na hutoa kutoka Kwake malipo makubwa.” (04:40)

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah, basi haitodhulumiwa nafsi yoyote ile kitu chochote kile. Na japokuwa ni uzito wa mbegu ya hardali, Tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu.” (21:47)

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri [hata kama ni] uzito wa chembe ya atomu basi ataiona, na yule atakayetenda shari uzito wa chembe ya atomu basi ataiona.” (99:07:08)

Tazama atomu inakuwa na uzito wa kiasi gani. Mtu akitoa swadaqah ya pesa moja, tonge moja au tende moja kumpa fakiri inakuwa atomu nyingi na kuwa na uzito mkubwa. Vipi kwa mwenye kutoa mapesa na mapesa na chakula kingi? Bila shaka atalipwa kwayo endapo atakuwa ni mwenye kumtakasia Allaah ni yake:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri [hata kama ni] uzito wa chembe ya atomu basi ataiona, na yule atakayetenda shari uzito wa chembe ya atomu basi ataiona.”

Imepokelewa vilevile kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba alitoa swadaqah ya punje ya zabibu ambapo akaulizwa uzito wake. Akasema:

“Punje hii itakuwa na uzito wa atomu kiasi gani?”[1]

Ninacholenga ni kwamba mtu asidharau swadaqah hata kama itakuwa kidogo. Muhimu atoe kiasi na uwezo wake. Atoe pesa moja, pesa mbili, tonge ya chakula ampe mwombaji, tende moja, tende mbili na kadhalika. Anas bin Maalik amesema:

“Mwanamke mmoja alikuja nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuomba akiwa na watoto wawili wakike. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anasema kuwa hawakupata nyumbani isipokuwa tende tatu peke yake. Akachukua zile tende tatu na kumpa yule mwombaji. Yule mwanamke akampa kila msichana tende moja na ile ya tatu akaichukua ili aile yeye. Lakini hata hivyo na ile tende ya tatu akawa amewagawia nayo wale watoto wakike wawili na yeye hakula kitu. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anaelezea kuwa kitendo kile kikamfurahisha. Pindi alipokuja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikamweleza ambapo akasema: “Hakika Allaah (Subhaanah) amemuwajibishia [mwanamke huyo] Pepo.”[2]

Hili ni kutokana na huruma hii aliokuwa nao juu ya wasichana wake na akawagawia tende zote na yeye hakula kitu. Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa kutoa swadaqah, ijapo itakuwa kwa kitu kidogo, ilimradi mtu ameitoa kwa nia nzuri, ndani yake ina kheri nyingi. Kilicho muhimu ni mtu atoe swadaqah kwa kile kitachowezekana. Mwenye uwezo wa 100, 1000, pesa moja, tende moja, tonge ya chakula, nguo na mfano wa haya mtu atoe swadaqah. Amesema  (Ta´ala):

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.” (64:16)

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah, basi haitodhulumiwa nafsi yoyote ile kitu chochote kile. Na japokuwa ni uzito wa mbegu ya hardali, Tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu.”

Allaah atuongoze sote.

[1] Ni kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na sio Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh). Ameipokea Ibn ´Abdil-Barr katika “al-Mustadrak” (1881) (08/602).

[2] al-Bukhaariy (1418) na Muslim (2630).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 28/10/2024