58. Du´aa ya kumwambia aliyepatwa na msiba

143 – Usamaah bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia:

“Tulikuwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mmoja katika wasichana wake alipomtumia mjumbe kumweleza kuwa mtoto wake wa kiume ameaga dunia. Akamwambia yule mjumbe kwamba arejee kwake na amweleze:

أَنَّ لِلَّهِ مَا أَخَذَ، وَلَهُ مَا أَعْطَى، وَكُلُّ شَيْءٍ عِنْدَهُ بِأَجَلٍ مُسَمًّى، فَمُرْهَا فَلْتَصْبِرْ وَلْتَحْتَسِبْ

“Ni Chake Allaah kile alichokichukua na ni Chake alichokitoa na kila kitu Kwake kina muda maalum.”

Mwamrishe avute subira na taraji malipo.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

144 – Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwa Abu Salamah ilihali macho yake yamemtoka ambapo akamfumba kisha akasema: “Roho inapochukuliwa inasindikizwa na macho.” Watu wakapiga makelele katika watu wake. Akasema: “Msijiombe dhidi ya nafsi zenu isipokuwa kwa kheri. Kwani Malaika huitikia “Aamiyn” kwa yale mnayoyasema.” Kisha akasema:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِأَبِي سَلَمَةَ وَارْفَعْ دَرَجَتَهُ فِي الْمَهْدِيِّينَ، وَاخْلُفْهُ فِي عَقِبِهِ فِي الْغَابِرِينَ، وَاغْفِرْ لَنَا وَلَهُ يَا رَبَّ الْعَالَمِينَ، وَافْسَحْ لَهُ فِي قَبْرِهِ، وَنَوِّرُ لَهُ فِيهِ

“Ee Allaah! Msamehe Abu Salamah, ipandishe daraja yake katika wale waliotangulia, mkaimu kwa kizazi chake katika wale aliowaacha, msamehe yeye na sisi, ee Mola wa walimwengu, mpanulie ndani ya kaburi lake na umtilie nuru ndani yake.”[2]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Ndani ya Hadiyth hii kuna ubainifu wa tanzia na matamshi ya rambirambi. Kwa hivyo unapotaka kumpa pole mfiliwa mwambie:

أَنَّ لِلَّهِ مَا أَخَذَ، وَلَهُ مَا أَعْطَى، وَكُلُّ شَيْءٍ عِنْدَهُ بِأَجَلٍ مُسَمًّى، فَمُرْهَا فَلْتَصْبِرْ وَلْتَحْتَسِبْ

“Ni Chake Allaah kile alichokichukua na ni Chake alichokitoa na kila kitu Kwake kina muda maalum.”

Namna hii ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa rambirambi msichana wake juu ya binti yake na akamwamrisha yule mjumbe amwambie namna hiyo.

Katika kisa hiki kumepokelewa kuwaelekeza waombee yaliyo na kheri. Du´aa zake zote (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni katika rambirambi.

[1] al-Bukhaariy (7377) na Muslim (923).

[2] Muslim (920).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 136-137
  • Imechapishwa: 15/11/2025