Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Mizani itawekwa mbele na yapimwe matendo ya waja:
فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ
“Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni wale ambao imekhasirika nafsi zao, [watakuwa] katika [Moto wa] Jahannam ni wenye kudumu.” (23:102-103)
Madaftari yataenezwa ambayo ndani yake kumeandikwa matendo. Kuna ambao watapewa madaftari yao kwa mkono wa kulia, na kuna ambao watapewa madaftari yao kwa mkono wa kushoto au nyuma ya mgongo wao, kama alivyosema (Subhaanahu wa Ta´ala):
وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا
”Na kila mtu Tumemuambatanishia majaaliwa ya matendo yake shingoni mwake na tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa, [ataambiwa]: “Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosheleze leo kukuhesabia dhidi yako.” (17:13-14)
Allaah atawafanyia hesabu viumbe. Atakaa chemba ma mja Wake muumini halafu atamfanya ayakubali madhambi yake, kama ilivyokuja ndani ya Qur-aan na Sunnah.
Kuhusu makafiri, hawatohesabiwa hesabu kwa njia hiyohiyo ya matendo mema na mabaya kupimwa, kwa sababu hawana mema yoyote. Badala yake matendo yao yatahesabiwa na wayajue na hivyo walipwe kwayo.
MAELEZO
Watasimama kwenda kwa Mola wa walimwengu na Allaah (Jalla wa ´Alaa) atawafanyia hesabu viumbe. Mizani itawekwa na matendo ya waja yapimwe. Yule ambaye mizani yake itakuwa na uzito huyo ndiye mwenye furaha na kufaulu. Ama yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu huyo ndiye mwangamivu.
Madaftari yatagawanywa na kusambazwa kati yao. Kuko ambao watapokea madaftari yao kwa mikono ya kulia na wengine watapokea madaftari yao kwa mikono ya kushoto au nyuma ya migongo yao, kama ilivyobainishwa katika Qur-aan.
Kuhusiana na makafiri hawatofanyiwa hesabu kwa njia ya mema na maovu yao kupimwa. Kwa sababu makafiri hawana mema yoyote. Lakini hata hivyo yatadhibitiwa matendo yao, wayakubali na halafu walipwe kwayo. Kwa msemo mwingine watatupwa Motoni. Matendo yao yatadhibitiwa, wayakubali na wayatambue. Baada ya hapo watupwe Motoni. Amesema (Ta´ala):
وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا
“Na wataendeshwa wale waliokufuru kuelekea [Moto wa] Jahannam makundi-makundi.” (39:71)
Itakuwa ni makundi baada ya makundi. Haya ni kutokamana na matendo yao machafu na kumkufuru kwao Allaah (´Azza wa Jall).
Ama watu wa Peponi wataingizwa Peponi kukirimiwa kikundi baada ya kutoka kwenye kiwanja cha Mkusanyiko wa hesabu na baada ya kupita juu ya Njia na kupitia kisimamo kirefu watachosimamishwa. Hapo ndipo sasa wataingizwa Peponi kwa kila mmoja kuwekwa makazi yake stahiki ambayo anayajua vyema zaidi kuliko makazi yake ya ulimwenguni. Hivyo wayatendea makazi yao ambayo Allaah amewaandalia baada ya kupitia hatua kadhaa zitatajwa huko mbele Allaah akitaka.
Siku ya Qiyaamah ni siku nzito. Ni sawa na miaka 50.000. Itakuwa ni siku nzito kwa makafiri na nyepesi kwa waumini. Amesema (Ta´ala):
أَصْحَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَئِذٍ خَيْرٌ مُّسْتَقَرًّا وَأَحْسَنُ مَقِيلًا
“Watu wa Peponi Siku hiyo wako katika makazi bora ya kutulia na mahali pazuri kabisa pa kupumzikia.” (25:24)
Watu wa Peponi watakuwa sehemu zao za starehe Peponi na watu wa Motoni watakuwa sehemu zao Motoni.
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 85-86
- Imechapishwa: 28/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)