Mja anapojisahau nafsi yake huacha kuyazingatia maslahi yake na hujishughulishwa na mengineyo. Matokeo yake huangamia na kuharibika – jambo lisiloepukika – kama mwenye shamba, bustani, mifugo au kinginecho, ambacho ufanisi wake uko katika kuendelea kukiendeleza na kukihudumia. Lakini yeye akakisahau na kukiacha na kujishughulisha na mambo mengine na kuharibu maslahi yake, basi bila shaka kitaangamia. Haya yakiwa ni mambo ambayo mtu mwingine anaweza kumsadia kuyahudumia badala yake, basi itakuwaje kwa nafsi yake ambayo hakuna mwingine atakayefanya kazi yake badala yake? Itakuwa ni uharibifu, kuangamia, kufeli na kunyimwa kila kheri. Huyu ndiye ambaye mambo yake yote yameparanganyika, yakamponyoka, yakampita na maslahi yake yakapotea. Yakazungukwa na sababu za kukatika kheri, kufeli na kuangamia. Hakuna njia ya kuokoka na hayo isipokuwa kwa kuendelea kumtaja Allaah (Ta´ala), ulimi kuendelea kuwa mbichi kwa Dhikr Yake na mja kuizingatia Dhikr hiyo kuwa kama uhai wake – asiyeweza kuishi bila hiyo – na kuwa kama chakula chake, ambacho akikikosa mwili wake huharibika na huangamia, kama maji wakati wa kiu kali, kama nguo wakati wa joto au baridi na kama makazi wakati wa baridi kali au upepo mkali wa joto. Basi inafaa kwa mja afanye kumtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika nafasi hiyo au kubwa zaidi. Basi kuko wapi kuangamia kwa roho, moyo wake na kuharibika kwake dhidi ya kuangamia kwa mwili wake na kuharibika kwake? Huu ni uharibifu wa lazima na mara nyingine hufuatiwa na ufanisi. Ama uharibifu wa moyo na roho ni uharibifu ambao hauna matumaini ya ufanisi wala mafanikio. Ingelikuwa kudumu na Dhikr hakuna faida nyingine isipokuwa hii pekee basi ingelitosha.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 105-106
  • Imechapishwa: 19/08/2025