Mwengine ni Thaabit bin Qays bin Shammaas (Radhiya Allaahu ´anh). Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Wakati iliposhuka Aayah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ

“Enyi walioamini! Msizinyanyue sauti zenu juu ya sauti ya Mtume na wala msiseme naye kwa sauti ya juu kama mnavyosemezana wenyewe kwa wenyewe kwa sauti za juu, yasije yakaporomoka matendo yenu nanyi hamhisi.”[1]

Thaabit bin Qays alikaa nyumbani kwake na akasema: “Mimi ni miongoni mwa watu wa Motoni.” Akajitenga mbali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza Sa´d bin Mu´aadh: “Ee Abu ´Amr! Thaabit ana nini? Anaumwa?” Sa´d akasema: “Ni jirani yangu na si mgonjwa kutokana na ninavyojua.” Hivyo akamwendea Sa´d na kumweleza maneno yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Thaabit akasema: “Kumeteremshwa Aayah na hakika nyinyi mnajua kuwa mimi ndiye ambaye nina sauti ya juu zaidi kuliko nyinyi mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mimi ni miongoni mwa watu wa Motoni.” Sa´d akaenda na kumweleza hayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Bali yeye ni katika watu wa Peponi.”[2]

[1] 49:02

[2] al-Bukhaariy (3613) na Muslim (187).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 136-137
  • Imechapishwa: 20/05/2026